Main Title

source : Parstoday
Jumatatu

8 Aprili 2024

20:17:30
1450088

ICJ kusikiliza kesi ya Nicaragua dhidi ya Ujerumani kwa kuunga mkono jinai za Israel

Majaji katika mahakama kuu ya Umoja wa Mataifa wataanza kusikiliza kesi iliyowasilishwa na Nicaragua ikiishutumu Ujerumani kwa kuunga mkono "mauaji ya kimbari" yanayotekelezwa na utawala wa Israel dhidi ya watu wa Palestina huko Gaza.

Kesi hiyo itaanza kusikiliza leo Jumatatu katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) huko The Hague. Mahakama hiyo huenda ikachukua wiki kadhaa kabla ya kutoa uamuzi wake wa awali.

Nicaragua imeitaka mahakama kutoa maagizo ya awali yanayojulikana kama hatua za muda, ikiwa ni pamoja na kwamba Ujerumani inapaswa kusitisha "mara moja"  msaada wake kwa Israel, haswa, msaada wake wa kijeshi hasa kutokana na kuwa msaada huo unaweza kutumika katika ukiukaji wa Mkataba wa Mauaji ya Kimbari na sheria za kimataifa.

Nicaragua inasema kuwa kwa kuipa Israel uungwaji mkono wa kisiasa, kifedha na kijeshi na kwa kulinyima ufadhili shirika la Umoja wa Mataifa la misaada kwa Wapalestina, UNWRA, "Ujerumani inawezesha utendaji jinai wa mauaji ya kimbari na  hivyo  imeshindwa katika wajibu wake wa kufanya kila linalowezekana kuzuia mauaji ya kimbari."

Mnamo Januari, ICJ ilichukua hatua za muda na kuamuru utawala wa Israel kufanya kila iwezalo kuzuia vifo, uharibifu na vitendo vya mauaji ya kimbari huko Gaza. Amri hizo zilitolewa katika kesi iliyowasilishwa na Afrika Kusini ikiishutumu Israel kwa kukiuka Mkataba wa Mauaji ya Kimbari.Wiki iliyopita, mahakama hiyo iliamuru Israeli kuchukua hatua za kuboresha hali ya kibinadamu huko Gaza, ikiwa ni pamoja na kufungua vivuko zaidi vya nchi kavu ili kuruhusu chakula, maji, mafuta na vifaa vingine katika eneo lililoharibiwa na vita.

Kesi ya leo katika mahakama hiyo ya kimatifa inakuja huku kukiwa na ongezeko la wito kwa madola ya Magharibi yanayoongozwa na Marekani kuacha kuikabidhi Israeli silaha.

Wapalestina wanakabiliwa na vifo na uharibifu huko Gaza huku mashambulizi yanayotekelezwa na Israel kwa himaya kamili ya Marekani katika eneo lililozingirwa yakiendelea kwa mwezi wa saba sasa.

Takriban raia 33,200  Wapalestina wameuawa katika mashambulizi hayo ya Israel tangu utawala huo ghasibu uanzishe vita vyake vya mauaji ya halaiki katika eneo hilo lililozingirwa Oktoba 7 mwaka jana.



342/