Main Title

source : Parstoday
Jumatano

10 Aprili 2024

15:49:50
1450457

Umoja katika medani ya Muqawama ni jinamizi jipya la utawala wa Israel

Sambamba na kuendelea mashambulizi ya jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Gaza na kukataa kukubali usitishaji vita, vikosi vya muqawama (mapambano ya Kiislamu) ndani na nje ya Palestina pia vimeongeza nguvu na wigo wa mashambulizi ya kujihami dhidi ya utawala huo katili.

Kuhusiana na suala hilo, vikosi vya mapambano ya Kiisalmu  nchini Iraq vimetangaza kuwa katika kipindi cha siku hivi karibuni  vimelanga shabaha tano muhimu na za kistratijia za utawala wa Kizayuni wa Israel.

Harakati ya Muqawama ya Iraq, kundi mwavuli la wapiganaji wa kupambana na ugaidi, katika taarifa yake ya Jumanne asubuhi ilitangaza kwamba imeshambulia  bandari muhimu ya mji  Ashkelon na maeneo mengine yanayokaliwa kwa mabavu na Israel kwa kutumia makombora na ndege za kivita zisizo na rubani.

Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Iraq lilichapisha picha za shambulio la kombora kwenye bandari ya mafuta ya Ashkelon, ambalo lilitekelezwa kwa kutumia kombora la umbali wa kilomita 1000 la Al-Arqub.

Saa moja baada ya taarifa yake ya kwanza, Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Iraq ilitangaza katika taarifa nyingine kwamba imeshambulia kwa mafanikio eneo lingine muhimu la Jeshi la Kizayuni, ikiwa ni pamoja na kambi ya anga ya Hatsarim iliyoko Beersheba, na itaendelea na operesheni hizo.

Wakati huo huo, Hizbullah ya Lebanon ililenga kwa makombora kambi ya Yoaf na kambi ya Kila inayomilikiwa na utawala wa Kizayuni.

Kanali ya 12 ya utawala wa Kizayuni wa Israel imeripoti kuwa makombora matano kutoka Lebanon yalipiga maeneo ya wazi ya Galilaya.
Vyombo vya habari vya Kiebrania vimekariri sana matamshi ya Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon katika hauli ya kumbukumbu ya kuuawa shahidi makamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) huko Syria na kutangaza kuwa, ujumbe jumla wa hotuba ya Nasrallah ni ujumbe mkali kwa Israel.

Wakati huo huo waungaji mkono wa utawala ghasibu wa Kizayuni wa Israel ambao wanahusika katika mauaji ya utawala huo ghasibu huko Gaza, hawajaepushwa na mashambulizi ya kujihami na kujikomboa ya vikosi vya muqawama na wamepokea maonyo makali dhidi ya kuendelea uungaji mkono wao wa kipofu kwa Israel.

Kuhusiana na suala hilo, akizungumza katika kikao cha wanahabari kilichorushwa hewani moja kwa moja kutoka mji mkuu wa Yemen, Sana'a siku ya Jumapili, Brigedia Jenerali Yahya Saree msemaji wa Jeshi la Yemen amesema vikosi vya nchi hiyo vimeishambulia meli ya mizigo ya Uingereza ya HOPE ISLAND katika Bahari ya Sham.