Main Title

source : Parstoday
Jumatano

10 Aprili 2024

15:54:58
1450465

Iran, mwenyeji anayefaa wa kuwahudumia wakimbizi

Kupitia taarifa, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesisitiza msimamo wa serikali ya Tehran wa kuendelea kuwahifadhi kwa ukarimu wahajiri na wakimbizi huku ikikanusha madai yanayotolewa na baadhi ya vyombo vya habari kuhusiana na kushinikizwa wakimbizi na raia wa kigeni nchini.

Kutokana na miaka mingi ya vita, kukaliwa kwa mabavu nchi zao na ukosefu wa usalama katika baadhi ya nchi zikiwemo Afghanistan, Iraq na Kuwait, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima imekuwa mwenyeji wa mamilioni ya raia wa nchi hizo katika miongo minne iliyopita.

Katika Vita vya Pili vya Dunia, Iran ilikaribisha nchini zaidi ya wakimbizi laki moja wa Ulaya, wakiwemo elfu 74 kutoka Poland waliochoshwa na vita. Mapokezi ya raia walioathirika na vita wa Azerbaijan na Armenia katika miaka ya karibuni pia yanatathminiwa katika mtazamo huo huo. Kwa hakika, watu wa Iran wamepokea wakimbizi kutoka nchi mbalimbali katika nyakati tofauti, kadiri kwamba wanahistoria, kwa mujibu wa kitabu kitakatifu cha Mayahudi, "Torati", wanasema maarufu zaidi kati ya wakimbizi hao ni hifadhi na himaya iliyotolewa na Mfalme Kourosh wa Iran mwaka 538 BC kwa Mayahudi waliokuwa chini ya udhibiti wa wafalme wa Babeli (Babylon).

Hata hivyo, baadhi ya vyombo vya habari vyenye chuki dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mara kwa mara huituhumu Tehran kuwa inawatendea visivyo wakimbizi hususan wa Afghanistan ili kupotosha fikra za waliowengi duniani kuhusu ukarimu na makaribisho ya Wairani kuhusiana na wakimbizi wanaotafuta hifadhi nchini. Kuhusiana na hilo, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Jamhuri ya Kiislamu karibuni hivi ilijibu uvumi unaoenezwa na maadui kuhusu wahajiri na raia wa kigeni na kusisitiza kuwa, msimamo wa Wizara hiyo kuhusu suala hilo uko wazi, na kwamba msaada wa kiwango cha juu wa Iran kwa wanaomba hifadhi na raia wa kigeni utaendelea.Taarifa hiyo inaeleza kuwa, suala la wahajiri na wakimbizi wa Afghanistan nchini Iran ni tatizo kubwa la kibinadamu lililosababishwa na uvamizi wa nchi za nje (Umoja wa Soviet na Marekani) dhidi ya Afghanistan. Inasema, licha ya kuwa siasa za Iran ni kuwasaidia wakimbizi, lakini hilo halina maana ya kuwapatia makazi ya kudumu nchini wala kutokabiliana na wakimbizi wanaoingia nchini kinyume cha sheria.

Katika miongo michache iliyopita, hali ya ndani ya Afghanistan iliyosababishwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe na uvamizi wa kigeni imepelekea mamilioni ya watu kukimbia nchi hiyo kwa lengo la kuokoa maisha yao. Wameziona nchi za Iran na Pakistan kuwa chaguo bora na la kwanza kutokana na masuala ya yanayowakutanisha pamoja raia wa nchi hizi kama vile lugha, dini utamaduni na vilevile ujirani wao.

Licha ya Umoja wa Mataifa na serikali zinazoingia madarakani Afghanistan kusifu mienendo mizuri ya Iran kuhusiana na wakimbizi wa nchi hiyo katika miongo minne iliyopita, baadhi ya vyombo vya habari na watu wenye chuki na Iran katika wiki za hivi karibuni wamekuwa wakidai kwamba juhudi zinazofanywa na Tehran kwa ajili ya kuwarejesha nyumbani wakimbizi haramu wa Afghanistan zinaashiria mabadiliko katika sera zake kuhusu wakimbizi hao.

Hii ni katika hali ambayo serikali ya Taliban huko Afghanistan, licha ya kupita miaka miwili ya utawala, haijaandaa mazingira yoyote ya kiusalama na kiuchumi kwa ajili ya kuwarejesha nyumbani raia wa nchi hiyo. Kwa vyovyote vile, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikiwahifadhi mamilioni ya wakimbizi wa Afghanistan kwa njia bora zaidi kwa zaidi ya miongo minne sasa, licha ya kukabiliwa na vikwazo vya kikatili vya nchi za Magharibi.

Wakimbizi wa Afghanistan nchini Iran sio tu wanaishi kwa amani bali wananufaika na suhula zote za elimu, masomo na afya na kuchanyanyika na raia wa Iran bila kubaguliwa. Hii ni katika hali ambayo wakimbizi wa Afghanistan katika nchi nyingine jirani wanaishi katika kambi za wakimbizi au katika maeneo maalumu ya wakimbizi, jambo ambalo linatambuliwa kuwa aina fulani ya udhalilishaji. Agizo la Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa ajili ya kupewa malezi bora watoto wote wa Afghanistan nchini Iran linahesabiwa kuwa miongoni mwa maamuzi muhimu zaidi katika utoaji huduma kwa wakimbizi, jambo ambalo ni la kupigiwa mfano katika ngazi za kimataifa na limekuwa likisifiwa mara kwa mara na Umoja wa Mataifa na taasisi nyingine zinazohusika na masuala ya wakimbizi.Inatupasa pia kusema kuwa, Uwepo wa idadi kubwa ya wakimbizi nchini unaitwisha serikali ya Iran gharama kubwa ya kifedha ambayo huongezeka maradufu kwa kutilia maanani kiwango cha suhula na huduma zinazotolewa na Iran kwa wakimbizi hao. Kwa kuzingatia hayo, kuna udharura wa Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi kuisadia serikali ya Iran katika kugharamia mahitaji ya wakimbizi. Hata hivyo msaada unaotolewa na shirika hilo katika uwanja huo ni mdogo sana na hauwezi kufanya lolote la maana. Kwa mujibu wa wataalamu, hivi sasa mgogoro wa Afghanistan umesahaulika kutokana na vita vya Ukraine, ambapo wakimbizi wa Afghanistan wanakabiliwa na siasa kali za ubaguzi hasa katika nchi za Ulaya, huku Iran ikiendelea kupokea na kuwahudumia maelfu ya wakimbizi kutoka Afghanistan.

342/