Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

12 Aprili 2024

19:22:28
1450808

Mauaji ya makamanda wa Muqawama na familia zao; ujumbe na matokeo yake

Utawala wa kizayuni wa Israel umefanya jinai nyingine na kuwauwa shahidi watoto na wajukuu wa Ismail Haniyeh, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas).

Mwezi wa saba unapita sasa tangu utawala wa Kizayuni wa Israel uanzishe vita na mauaji ya kimbari dhidi ya wakazi wa Ukanda wa Gaza huko Palestina. Hata hivyo utawala huo umefeli na kushindwa kutimiza malengo yake ya kijeshi katika vita dhidi ya Gaza. Baada ya Israel kushindwa kutimiza malengo yake ya kijeshi sasa umejielekeza katika kuwauwa kigaidi makamanda wa makundi ya Muqawama na familia zao. 

Mauaji hayo ya kigaidi dhidi ya makamanda wa muqawama na ndugu wa familia zao yana jumbe kadhaa. Ujumbe mkuu na muhimu ni kwamba, utawala wa Kizayuni wa Israel ni utawala wa kigaidi. Utawala huo ni baba wa kambo wa magaidi na una uzoefu na tajiriba ya juu katika kutekeleza mauaji ya kigaidi. 

Ujumbe mwingine ni kuwa, utawala wa Kizayuni umeshindwa kukabiliana na wanamapambano katika medani ya vita huko Gaza. Ni wazi kuwa, kushindwa katika medani ya vita kumeifanya Tel Aviv iwachukia makamanda wa Muqawama. Kuhusiana na suala hilo, harakati ya Jihad Islami ya Palestina imetuma ujumbe wa taazia na kutoa mkono wa pole kufuatia kuuliwa shahidi watoto wa kiume na wajukuu wa Ismail Haniya na kutangaza kuwa: Mauaji hayo ya kioga yanathibitisha kuwa adui yuko katika mkanganyiko kutokana na kushindwa kufikia malengo yake haramu katika uwanja wa vita; hivyo anafanya kila awezalo ili kufidia kushindwa kwake kwa kuwauwa kigaidi watoto wa wanamapambano wa ukombozi na ndugu wa familia zao. 

Ujumbe mwingine muhimu ni kuwa jinai za Israel zinathibitisha uongo wa madai wa kutetea haki za binadamu yanayotolewa na madola ya Magharibi. Hakuna hata nchi mmoja kati ya hizo za Magharibi zinazojinadi kuwa watetezi wa haki za binadamu dunia iliyolaani jinai hiyo ya Israel ya kuwauwa shahidi watoto na wajuu wa Ismail Haniyeh, na nchi hizo zinaendelea kuuhami na kuukingia kifua  utawala huo ghasibu. Kuhusiana na suala hilo, Meja Jenerali Mousavi, Mkuu wa Majeshi ya Iran amesema katika ujumbe wake kwa Ismail Haniyeh kuwa, kimya na uungaji mkono wa pande zote wa wale wanaodai kutetetea haki za binadamu ndiyo sababu kuu inayoutia kiburi utawala haramu wa Israel utekeleze jinai za kutisha kama hiyo. Ujumbe mwingine muhimu ni kwamba, propaganda za utawala wa Kizayuni na waungaji mkono wake kuhusu makamanda wa Muqawama na familia zao zimethibitika kuwa za uongo. 

Katika kipindi cha miezi 6 iliyopita ambapo zaidi ya Wapalestina 33,000 wameuawa shahidi na wengine zaidi ya 75,000 kujeruhiwa kutokana na vita vya Gaza; moja ya mihimili ya propaganda za Wazayuni na vyombo vya habari vya Magharibi ni kwamba watu wa Gaza ni wahanga wa vita hivyo, lakini watoto na familia za makamanda wa Muqawama zinaishi katika hali nzuri nje ya Gaza. Kuhusiana na hili, Ismail Haniyeh alisema baada ya kuuawa kishahidi  wanawe na wajukuu wake kwamba: Wanangu wamekuwa wakiishi pamoja na raia wengine wa Ukanda wa Gaza na hawakuondoka katika eneo hilo. "Wapalestina  na wakazi wote wa Gaza wamelipa gharama kubwa kwa kutoa damu ya watoto wao, na mimi ni mmoja wao. Takriban watu 60 wa familia yangu wameuawa shahidi sawa kabisa na  Wapalestina wote, na hakuna tofauti yoyote iliyopo miongoni mwao."  

Swali linaloulizwa hapa ni kuwa, jinai hii itakuwa na taathira gani? Taathira muhimu zaidi ya jinai hii ni kuimarika mapambano ya ukombozi ya wanamapambano wa Palestina na kuendeleza vita dhidi ya Wazayuni maghasibu katika miaka ijayo. Jihad Islami ya Palestina imesisitiza katika taarifa yake kuwa kuwauwa kigaidi viongozi, makamanda, watoto na familia za wamamuqawama hakutakuwa na matokeo yoyote isipokuwa kuzidisha azma, kuwafanya ngangari zaidi wananchi wa Palestina na kuzidisha mwamko wa Wapalestina. Ismail Haniyeh pia amesisitiza kuwa, kwa maumivu haya na damu zilizomwagika tunajenga matumaini, mustakbali na uhuru kwa taifa, kadhia ya Palestina na taifa letu."