Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

12 Aprili 2024

19:23:54
1450810

Kuongezeka kimataifa uungaji mkono kwa kampeni ya kususia bidhaa za Israeli

Huku mauaji ya kimbari yakiwa yanaendelea kufanywa na utawala haramu wa Israel dhidi ya watu wa Gaza, nchi nyingi duniani zinaendelea kujiunga na kampeni ya kususia bidhaa za Israel na vilevile za makampuni mengi ya Kimarekani yanayouunga mkono utawala huo wa kibaguzi.

Katika hatua ya hivi punde, migahawa ya Denmark imeacha kutumia bidhaa za Coca-Cola katika kulalamikia hatua za Marekani na Israel dhidi ya watu wa Gaza. Waandaaji wa kampeni hiyo nchini Denmark wanasema, mzalishaji mkuu wa vinywaji hivyo (Marekani) anasaidia ukandamizaji wa utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina. Mmoja wa wanachama wa kampeni hiyo, Freddie Ekbolut, anasema: 'Kwa kuondoa bidhaa za Coca-Cola kwenye orodha zao za vinywaji, washiriki wa kampeni hii wanaonyesha mshikamano na huruma yao kwa Palestina.'

Kabla ya hapo, matawi mengi ya McDonald yalikuwa tayari yamesusiwa na watumiaji katika nchi nyingi za Kiislamu na hata za Ulaya. Kampuni hii ambayo ina matawi mengi katika Palestina inayokaliwa kwa mabavu (Israel), moja kwa moja na kwa njia isiyo ya moja kwa moja inaunga mkono mashambulizi ya kikatili yanayofanywa na utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza. Suala hili limepelekea watumiaji wengi wa bidhaa za McDonald's kususia bidhaa hizo na kuziweka kwenye 'orodha nyeusi', wakikosoa uungaji mkono wake kwa jinai zinazofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina wasio na hatia na hasa wanawake na watoto. Kuhusiana na hilo, McDonald's ilitangaza wiki iliyopita kwamba itaipokonya kampuni ya Kizayuni, vibali vya umiliki wa matawi yake yote katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu (Israel). Huku jinai za Israel zikiwa zinaendelea kufuatia kushindwa mazungumzo ya kuhitimisha vita vya Gaza, wigo wa kususia kiuchumi bidhaa za Wazayuni sio tu umepanuka, bali sasa unayajumuisha mashirika ya Kimarekani.

Kwa hakika Marekani ndiyo muungaji mkono mkubwa zaidi wa Israel katika mauaji ya Wapalestina tangu kuanza vita vya Gaza na inaendelea kutoa uungaji mkono wa kifedha, kijeshi na kisiasa kwa utawala huo wa Kizayuni bila kusita. Kiasi cha msaada wa kijeshi wa Marekani kwa Israel ni takriban dola bilioni 3.8 kwa mwaka. Katika vita vya Gaza, Washington inautumia utawala huo katili kila aina ya ndege za kivita, mabomu yenye uharibifu mkubwa na silaha za kisasa kabisa, misaada ambayo inaendelea bila kusita.

Aidha Marekani imezuia kivitendo kumalizika vita vya Gaza kwa kuvuruga na kupinga maamuzi ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Kuhusiana na hilo, Bernie Sanders, seneta wa kujitegemea wa Marekani, ameandika kwenye mtandao wa X kama ifuatavyo: 'Ni lazima tusitishe ushirikiano wetu na Israel. Msitume tena mabomu Israel.'

Idadi ya mashahidi huko Gaza imepindukia watu elfu 33 ambapo ripoti za kimataifa zinasema maafa ya watu katika ukanda huo na hasa ya wanawake na watoto ni ya kutisha. Cindy McCain, Mkurugenzi wa Mpango wa Chakula Duniani ameonya kuhusiana na jambo hili kwamba: Watoto huko Gaza wanakufa kwa njaa, na wale ambao bado wako hai wamedhoofika sana kutokana na umaskini na uhaba mkubwa wa chakula, ambapo miili yao haipati virutubisho muhimu.
Vita vya Gaza na uungaji mkono wa Marekani kwa utawala haramu wa Israel unaendelea huku maafisa wa Washington wakikiri kushindwa utawala huo katika vita hivyo. Kuhusiana na hilo, Rais Joe Biden wa Marekani katika matamshi yanayokinzana na utendaji kazi wake amedai kuwa, anatofautiana kimtazamo na Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni kuhusu vita vya Gaza. Wakati huo huo amekiri kuwa siasa za Israel huko Gaza zimeshindwa. Licha ya maonyo na maombi yote ya kusitishwa vita katika ukanda huo, lakini utawala wa Kizayuni ungali unaendeleza jinai zake dhidi ya watu wa eneo hilo ambapo uungaji mkono wa Marekani kwa utawala huo ghasibu pia unaendelea, jambo ambalo limewafanya wananchi wa nchi mbalimbali za dunia kuanzisha kampeni tofauti za kiuchumi na kisiasa kwa ajili ya kuonyesha kuchukizwa kwao na siasa za Israel za kutaka kukiangamiza kizazi kizima cha Wapalestina kwa uungaji mkono kamili wa Washington. Kususiwa bidhaa za Coca-Cola nchini Denmark pia kumetimia katika mwelekeo huo.

342/