Main Title

source : Parstoday
Jumapili

14 Aprili 2024

19:32:13
1451297

Kukiri Wazayuni kuhusu uwezo mkubwa wa kistratijia wa Iran

Viongozi wa utawala wa Kizayuni wamekiri kutokuwa na uwezo wa kukabiliana na nguvu na uwezo mkubwa wa kistratijia wa Iran.

Ndege za kivita za utawala wa Kizayuni Jumatatu iliyopita tarehe Mosi Aprili zilishambulia kwa makombora ubalozi mdogo wa Iran katika mtaa wa al Mazzeh huko Damascus mji mkuu wa Syria; ambapo watu 13 wakiwemo wanadiplomasia saba na washauri wa kijeshi wa Iran waliuawa shahidi. Viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wamesisitiza kuuadhibu utawala wa Kizayuni kwa jinai yake hiyo na wametangaza kuwa hatua ya kulipiza kisasi itakuwa kali.  Matokeo ya hatua za kulipiza kisasi zinazotarajiwa kuchukulia na Iran katika siku za karibuni yamezitia hofu baraza la mawaziri la utawala wa Kizayuni; ambapo vyombo vya habari vya utawala huo vimeashiria suala hili katika ripoti zao. Kanali ya 12 ya televisheni ya utawala wa Kizayuni imetangaza kuwa Israel imeitisha kikao cha usalama kilichohudhuriwa na Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa utawala huo na Yoav Galant Waziri wa Vita, Benny Gantz Waziri wa zamani wa Vita wa utawala wa kizayuni ambaye pia ni mwakilishi wa sasa wa Baraza la Vita na Gadi Eisenkot mjumbe wa Baraza la Vita la utawala wa Kizayuni. Kikao hicho cha usalama cha baraza la mawaziri la utawala wa Kizayuni kimefanyika kwa lengo la kuchunguza namna  Iran itakavyolipiza kisasi na njia za kukabiliana na hatua hiyo. 

Gazeti la lugha ya Kiibrania la Maarivc Ijumaa lilichapisha matokeo ya uchunguzi wa maoni uliofanika katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na kuandika: Hisia hasi zinatawala miongoni mwa asilimia  60  ya wakazi wa maeneo yanayokaliwa kwa mabavu (Israel); huku asilimia 24 wakiwa wamekata tamaa, na asilimia 23 ya Wazayuni wamekumbwa na wahka. 

Mahesabu kombo ya baraza la mawaziri la vita la Netanyahu yameusababishia utawala huo gharama zisizoweza kufidiwa baada ya makundi ya mapambano ya ukombozi ya Palestina kutekeleza oparesheni ya kushtukiza ya Kimbunga cha Al Aqsa Oktoba 7 mwaka jana. Makundi ya muqawama ya Palestina pamoja na makundi mengine ya muqawama katika nchi nyingine kama vile Iraq, Lebanon na Yemen yametoa kipigo kisichoweza  kufidiwa kwa utawala wa Kizayuni na muitifaki wao mkuu katika eneo la Mashariki ya Kati yaani Marekani; kipigo ambacho Wazayuni na Wamarekani wameshindwa kurudisha mapigo.  Kushambuliwa ubalozi mdogo wa Iran huko Damascus, ni sehemu nyingine ya hatua za jinai za utawala wa Kizayuni, iliyotekelezwa kinyume cha sheria za kimataifa. Utawala wa Kizayuni ambao umekata tamaa katika kukabiliana na vikosi vya wanamuqawama na huku ukiwa na lengo la kuibua hali ya wasiwasi na machafuko katika eneo hili umeshambulia moja ya maeneo ya kidiplomasia ambalo licha ya kuwa na kinga ya kisheria linahesabiwa kuwa sehemu ya ardhi ya nchi. Viongozi wapenda vita wa utawala ghasibu wa Kizayuni wanaendelea kuzusha mgogoro na kujaribu kuzusha vita kwa kutumia na kunufaikka na himaya na uungaji mkono endelevu na wa pande zote wa Marekani na nchi za Magharibi na pia vyombo vya habari vya Magharibi vinavyohalalisha jinai za Israel huko Ukanda wa Gaza. Hata hivyo vitendo hivi visivyo vya kawaida havina taathira tena na waungaji mkono wa utawala wa Kizayuni pia wanajaribu kutenganisha mahesabu yao na Tel Aviv. Hatua za kimkakati za Iran hususan baada ya kimbunga cha operesheni ya Al-Aqsa katika eneo zimepelekea kutengwa zaidi utawala wa Kizayuni. Makundi ya muqawama yamekuwa nguvu yenye taathira katika matukio ya eneo hili; na utawala wa Kizayuni umeshindwa kukabiliana pakubwa na operesheni na uwezo wa makundi ya muqawama kutokana na uungaji mkono endelevu na wenye taathira wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Nchi za eneo pia kwa kuzingatia matukio mapya na nafasi ya uharibifu ya utawala wa Kizayuni hazina tena imani na utawala huo na waungaji mkono wake yaani Marekani na nchi za Magharibi. Nafasi ya Iran hii leo ina taathira kubwa sana katika matukio ya eneo hili kwa kadri kwamba Wazayuni pia wamekiri kuwa wametengwa, na kuwa hawawezi kukabiliana na Iran. 

342/