Main Title

source : Parstoday
Jumapili

14 Aprili 2024

19:35:45
1451303

Katika barua kwa Papa, Erdogan ataka Ubinadamu ukomeshe ukiukaji zaidi wa sheria unaofanywa Ghaza

Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki ametoa wito kwa watu duniani kote kuzungumza dhidi ya mashambulizi ya kinyama ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya hospitali, skuli, misikiti na makanisa katika Ukanda wa Ghaza, Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Katika barua aliyomwandikia Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis Erdogan amesema: "Ubinadamu lazima uzuie ukiukaji zaidi wa sheria za kimataifa unaofanywa huko Ghaza", akisisitiza kwamba watu wasio na hatia na miundomsingi ya kiraia haipaswi kulengwa kamwe, hata wakati wa vita.

Huku akisisitiza kwamba mauaji ni marufuku katika imani zote zinazotokana na Nabii Ibrahim AS, Rais wa Uturuki amesema ubinadamu "lazima upaze sauti yake dhidi ya uripuaji wa makusudi wa hospitali, skuli, misikiti na makanisa ambayo hayapaswi kukiukwa, hata wakati wa vita".Erdogan ameendelea kueleza katika barua yake kwamba kuleta amani na utulivu wa kudumu katika Mashariki ya Kati hakuwezekani bila ya kutatuliwa kwa haki wa suala la Palestina na Israel.

Rais wa Uturuki amesisitiza katika barua yake hiyo kwa Papa akisema: "nchi huru ya Paletina yenye mamlaka kamili ya kujitawala na iliyounganishwa kijiografia na mipaka ya 1967, na Baitul Muqaddas Mashariki ikiwa ndio mji mkuu wake, lazima idhihirike na kuchukua nafasi yake katika mfumo wa kimataifa kama mwanachama mwenye haki sawa wa jamii ya kimataifa".../



342/