Main Title

source : Parstoday
Jumanne

16 Aprili 2024

18:28:38
1451868

Trump, rais wa kwanza wa zamani Marekani kuhukumiwa katika kesi ya jinai

Kesi ya Donald Trump katika mashtaka ya jinai ilianza jana, Jumatatu, mjini New York na kumfanya kuwa rais wa kwanza wa zamani wa Marekani kufika mbele ya mahakama ya jinai kujibu mashtaka yanayohusiana na kulipa pesa kwa mwigizaji wa filamu za ngono ili kumnyamazisha na kumtaka afiche uhusiano wake wa kingono na mwanamke huyo.

Duru za Marekani zinasema kesi hiyo yumkini ikaathiri azma yake ya kuwania urais na kurejea tena Ikulu ya White House.

Awali jaji wa mahakama hiyo alikuwa amemuonya Trump kwamba atalazimika kuhudhuria kesi katika mahakama ya Manhattan kila siku, vinginevyo atakamatwa. Jaji huyo pia alimuonya Trump dhidi ya majaribio yake ya mara kwa mara ya kuvuruga vikao vya mahakama kwa kusambaza machapisho ya uchochezi kwenye mitandao ya kijamii na kulipuka kwa hasira wakati wa vikao vya kesi yake.

Trump anakuwa rais wa kwanza wa zamani katika historia ya Marekani kufika mbele ya mahakama katika kesi ya jinai, katika kesi inayoweza kusababisha kifungo cha jela na hivyo kubadili uwiano wa kampeni za uchaguzi wa urais ambazo bilionea huyo anaendesha kama mgombea wa Chama cha Republican.

Iwapo Trump atapatikana na hatia, atakabiliwa na kifungo cha juu zaidi cha miaka 4 jela, lakini bado ataweza kushika wadhifa wa urais. Hata hivyo kura ya maoni iliyofanywa na mashirika ya Reuters/Ipsos imeonyesha kuwa hukumu ya kumtia hatiani Trump inaweza kutatiza safari yake ya kurejea White House.

342/