Main Title

source : Parstoday
Jumamosi

20 Aprili 2024

20:06:18
1452777

UN: Moto wa vita vya Sudan unachochewa na silaha zitokazo nje za wakiukaji wa vikwazo

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Masuala ya Kisiasa na Ujenzi wa Amani, Rosemary Anne DiCarlo ameliambia Baraza la Usalama kwamba vita nchini Sudan vimesababisha "hali mbaya ya kiwango cha kipekee" inayochochewa na silaha kutoka kwa waungaji mkono wa kigeni ambao wanaendelea kukiuka vikwazo vya Umoja wa Mataifa

Bi DiCarlo amesema: "kama pande zote zimeweza kuendeleza makabiliano yao, kwa sehemu kubwa ni kutokana na usaidizi wa nyenzo wanazopata kutoka nje ya Sudan". Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amefafanua kwa kusema: "wahusika hawa wa nje wanaendelea kukiuka sheria ya vikwazo iliyowekwa na Baraza la Usalama ili kuunga mkono suluhisho la kisiasa, na hivyo kuchochea mzozo. Hii ni kinyume cha sheria, ni kinyume cha maadili na lazima ikomeshwe." Sheria ya vikwazo iliyowekewa Sudan kulingana na azimio nambari 1591 inazitaja pande zote zilizohusika katika mzozo wa Darfur ambao ulizuka mwanzoni mwa miaka ya 2000. Inajumuisha marufuku ya silaha na risasi pamoja na kuzuia mali za wahusika.Mohamed Ibn Chambas, mwenyekiti wa jopo la Umoja wa Afrika linalohusika na Sudan na mwakilishi mkuu wa mpango wa umoja huo uitwao Silence the Guns in Africa, ameutaja uingiliaji kutoka nje kuwa "sababu kubwa inayovuruga juhudi zote mbili za mazungumzo ya kusitisha mapigano na za kukomesha vita".

Japokuwa si DiCarlo wala Chambas ambaye amewataja wahusika hao wa nje ya Sudan lakini ripoti zinasema, Saudi Arabia, Muungano wa Falme za Kiarabu UAE na Misri zinahusika katika kuendeleza vita nchini Sudan.

Licha ya juhudi kadhaa zilizofanywa hadi sasa ndani ya bara la Afrika na nje yake ili kurejesha amani nchini humo vita na mapigano yangali yanaendelea, yakihusisha Jeshi linaloongozwa na Jenerali Abdel Fattah al-Burhani na Vikosi vya Usaidizi wa Haraka RSF, vinavyoongozwa na Mohammed Hamdan Dagalo.../


342/