Main Title

source : Parstoday
Jumatatu

22 Aprili 2024

15:55:46
1453276

Rais wa Iran aendelea na ziara ya siku mbili nchini Pakistan kuboresha usalama na mahusiano ya kibiashara

Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran anaendelea na ziara yake ya siku mbili nchini Pakistan kwa lengo la kuimarisha usalama na uhusiano wa kibiashara baina ya nchi hizi jirani.

Rais Raisi amewasili mjini Islamabad leo Jumatatu kwa ziara rasmi akiongoza ujumbe wa ngazi ya juu wa kisiasa na kiuchumi. Akitoka Pakistan ataelekea nchini Sri Lanka kwa ziara hiyo hiyo ya kikazi.

Waziri Mkuu wa Pakistan Shehbaz Sharif amempokea rasmi rais wa Iran katika sherehe ambayo imeambatana na kulikagua jeshi la Pakistan kwa heshima yake. 

Mara baada ya sherehe hizo, Raisi na Sharif wamefanya mazungumzo ya faragha. Ratiba nyinyine kwa leo ilikuwa ni Rais wa Iran na Waziri Mkuu wa Pakistan kuongoza kikao cha wajumbe wa ngazi za juu wa nchi hizo mbili.

Kabla ya kuondoka Tehran kuelekea Islamabad leo asubuhi, Sayyid Ebrahim Raisi alisema, Iran inauchukulia usalama wa Pakistan kuwa ni usalama wake, kwa hivyo kuimarishwa usalama kwenye mpaka wa pamoja na Pakistan kutanufaisha mataifa yote mawili.

Akiashiria mtazamo wa pamoja wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Pakistan katika uga wa haki za binadamu, utetezi wa watu wanaodhulumiwa wa Palestina na mapambano dhidi ya ugaidi, Raisi alisema: katika mwendelezo wa sera ya ujirani mwema na kustawisha uhusiano na nchi za Kiislamu, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina hamu ya kukuza uhusiano na Pakistan na katika safari hiyo masuala mbalimbali yakiwemo ya kiuchumi na kibiashara, masuala ya nishati na mipaka yatajadiliwa na pande mbili.

Dakta Raisi ameeleza pia kuwa kiwango cha uhusiano wa kiuchumi kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Pakistan si cha juu kama kiwango cha uhusiano wa kisiasa, na akabainisha lengo la kufikiwa kiwango cha dola bilioni 10 katika mabadilishano ya kibiashara na kiuchumi, kwa kuzingatia uwezo mkubwa wa nchi mbili katika uwanja huo.

342/