Main Title

source : Parstoday
Jumatatu

22 Aprili 2024

15:56:38
1453278

Rais wa Iran awasili Pakistan katika ziara ya kuimarisha uhusiano wa kibiashara na usalama

Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amewasili katika mji mkuu wa Pakistan Islamabad katika ziara rasmi ya kikazi yenye lengo la kuimarisha usalama na uhusiano wa kibiashara kati ya nchi mbili.

Akiongoza ujumbe wa ngazi ya juu wa kisiasa na kiuchumi, Rais Raisi amewasili Islamabad mapema leo katika kituo cha kwanza cha ziara yake ya kuzitembelea nchi mbili itakayomfikisha pia Sri Lanka. Katika uwanja wa ndege, Rais wa Iran amelakiwa na Waziri wa Nyumba na Ujenzi wa Pakistan Mian Riaz Hussain Pirzada na maafisa kadhaa wa nchi hiyo. Waziri Mkuu wa Pakistan Shehbaz Sharif atamkaribisha rasmi baadaye Rais Raisi kisha pande hizo mbili zitafanya mkutano wa faragha.Kabla ya kuondoka Tehran kuelekea Islamabad leo asubuhi, Seyyed Ebrahim Raisi alisema, Iran inauchukulia usalama wa Pakistan kuwa ni usalama wake, kwa hivyo kuimarishwa usalama kwenye mpaka wa pamoja na Pakistan kutanufaisha mataifa yote mawili.

 Akiashiria mtazamo wa pamoja wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Pakistan katika uga wa haki za binadamu, utetezi wa watu wanaodhulumiwa wa Palestina na mapambano dhidi ya ugaidi, Raisi alisema: katika mwendelezo wa sera ya ujirani mwema na kustawisha uhusiano na nchi za Kiislamu, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina hamu ya kukuza uhusiano na Pakistan na katika safari hiyo masuala mbalimbali yakiwemo ya kiuchumi na kibiashara, masuala ya nishati na mipaka yatajadiliwa na pande mbili.

Dakta Raisi ameeleza pia kuwa kiwango cha uhusiano wa kiuchumi kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Pakistan si cha juu kama kiwango cha uhusiano wa kisiasa, na akabainisha lengo la kufikiwa kiwango cha dola bilioni 10 katika mabadilishano ya kibiashara na kiuchumi, kwa kuzingatia uwezo mkubwa wa nchi mbili katika uwanja huo.../

342/