Maana ya kifo:
Katika vitabu vya lugha, kifo kinafahamika kama:Kutoka uhai,kutokuwa na hisia, au kumaliza umri wa kuishi.(Mauti), Death.
Baadhi ya maneno yenye kufanana kimuundo wa kisarufi na kifo ni: Faraka, Fariki,Farakana:ikiwa na maana ya utengano.;
Mitazamo ya wanafalsafa:
Sirkatundu nikiwa kama mtu wa tafakuri na mwanafalsafa mchanga sina budi kwanza kuelezea mtazamo wangu kuhusu kifo nakisha nitaelezea mitazamo ya wakuu.
Mtazamo wangu ni kwamba: Kabla ya kuongelea kifo ambacho ni kama matokeo yanayotokea kwa mwanadamu, inabidi tufahamu uhalisia wa mwanadamu.
Je, Uhalisia wa mwanadamu ni mwili wake? Kiasi kwamba sehemu ya mwili ikipungua au kutoweka je? itamaanisha kutoweka,kupungua sehemu ya ubinadamu wake?
Jibu ni la,! Hasha uhalisia wa mwanadamu si mwili bali roho na nafsi. Hivyo kuwa na mapungufu ya mwili hakumaanishi kuwa na mapungufu ya ubinadamu.
Hivyo utengano wa mwili na roho haumanishi kuwa ndio mwisho wa maisha, bali ni mwanzo wa maisha mapya.
Maisha ya dunia ni maisha ya maada hivyo tunahitaji mwili kuishi katika ulimwengu wa maada hivyo muda unapofika wasisi kuachana na maisha ya maada tunauacha mwili, ambao ulikuwa ni kwa ajili ya matumizi ya muda mfupi na kubakia na asili yetu ambayo ni nafsi.
Hivyo hakuna maana kuogopa kifo kwani hiyo ni sababu ya sisi kurudi kwenye asili yetu na hakimaanishi mwisho wa maisha bali ni mwanzo wa mapya yasiyohitaji mwili.
Sasa maisha hayo utayapa jinalolote iwe kuzimu, iwe peponi, iwe popote pale ila ni maisha mengine na si mwisho wa maisha. Tunaogopa maisha hayo kwa sababu hatuyajui yakoje, kama vile ambavyo mtoto tumboni hajui maisha ya dunia vivyo hivyo sisi hatujui maisha ya baada ya kifo..
Ni muhimu kuashiria kwamba: watu wengi hudhani kwamba uhalisia wa mwanadamu ni mwili wake, hufikia hata wengine kujifahirisha kwa uzuri wa miili na maumbo yao. Ama hakika huu ni upofu kwani ni sawa na kujifahirisha kwa nyumba yakupanga ambapo muda ukifika utaiacha na kuondoka:Mwili hudhurika, mwili huzeeka, mwili huchoka, mwili huharibika na kubadilika kuwa mchanga, bali nafsi hubakia daima.
Pia ni upumbafu kujifaharisha kwa kitu ambacho hauna hiari nacho, kama kujifaharisha kwa mwili ambao umepewa tu na wala hukuhangaika kuutafuta, kama elimu, mali na vinginevyo.
Mwanafalsa wa Roma (Italia) aitwaye Seneca -ambaye aliishi miaka minne kabla ya kuzaliwa Kristo na kufariki wa 65 baada ya kuzaliwa Kristo- katika makala yake iitwayo “On Asthma and Death” anakizungumzia kifo akisema:
“Kufa ni kutokuwepo hii inamanisha kwamba, ambacho kilikuwepo kabla yangu kitakuwako tena baada yangu. Kama kuna maumivu au mateso katika hali hii ya kutokuwepo basi ni lazima pia kulikuwa na mateso au maumivu kabla ya kuzaliwa kwetu( kwani hatukuwepo pia), ukweli ni kwamba hatukusikia maumivu wala taabu yeyote kabla ya uwepo wetu, na vivyo hivyo ndivyo itavyokuwa wakati wa kuondoka kwetu.
Nawauliza kwamba, ati usingemwona kuwa ni kingunge wa wapumbavu, yule anayeamini kwamba taa iko katika hali mbaya zaidi baada ya kuzimwa kuliko muda wa kuwashwa?
Uhai wetu ni kama taa, huwashwa na kuzimwa . na kipindi cha maumivu,taabu na mashaka ni wakati taa imewashwa si kabla ya kuwashwa wala si baada ya kuzimwa. Hivyo katika pande zote mbili -kabla ya kuwashwa na baada ya kuzimwa - kuna amani isiyo na kikomo”
Mwanafalsafa huyu mkongwe katika makala yake mnyingine iitwayo: “On Taking One’s Own Life” anazungumzia kifo akisema:
“Hakuna mtu ambaye ni mpumbavu kiasi cha kutojua kwamba kuna siku tutakufa. Pamoja na ufahamu huu wote, wakati wa kufa unapokaribia bado kuna watu wengi huogopa, wakitetemeka na kuhuzunika. Je usingemwona kuwa ni mpumbavu kabisa mtu ambaye anahuzunika, kwa sababu ati hakuwepo miaka elfu moja iliyopita?
Na Je huoni kuwa ni mpumbavu kabisa mtu ambaye ana anaogopa na kuhuzunika kwa sababu hatakuwepo miaka elfu moja ijayo kutoka sasa?
Yote ni sawa: hutakuwepo na hukuwepo. Vipindi vyote hivi viwili si vyako.”
Mtazamo mwingine umetolewa na Epicurus mwanafalsafa wa Ugiriki aliyeishi mwaka 270 kabla ya Kristo. Mwanafalsafa huyu alitoa mchango mkubwa sana katika maendeleo ya Sayansi kutokana na mafundisho yake ya kutoamini vitu hovyo hovyo, hasa kabla ya kuvipima na kuvichunguza kiundani. Mwanafalsafa huyu anasema kwamba: lengo kuu la falsafa lilikuwa kuleta furaha na maisha ya utengamano , maisha yasiyo na maumivu wala hofu.
Katika kukundolea hofu ya kifo mwanafalsafa huyu Epicurus anatoa hoja ifuatayo:
• Unapokuwapo kifo hakipo; na kisichokuwepo hakiwezi kukudhuru, halikadhalika Kifo kinapokuwepo wewe haupo; na kisichokuwepo hakiwezi kudhuriwa.
• Ni upumbavu kuogopa ambacho hakiwezi kukudhuru. Ni upumbavu pia kuogopa ambacho hakiwezi kudhuriwa.
Katika wakati wowote ule imma wewe unakuwepo au kifo kinakuwepo, Kwa hivyo katika wakati wowote ama kifo hakiwezi kukudhuru, au huwezi kudhuriwa na kifo.
Hii ni mitazamo ya baadhi ya wanafalsafa na watu wa tafakuri kuhusi kifo, hivyo sidhani kama ni busara kuendelea kuugopa kifo .
FAIDA ZA KIFO:
• Kufahamu umuhimu na thamani Uhai: kifo kimekuwa ni sababu ya watu kujali na kufahamu umuhimu wa maisha na uhai.
• Kufahamu umuhimu wa muda: kifo kimekuwa ni sababu ya watu kufahamu umuhimu wa muda na kutoupeteza bure. Ifahamike kwamba ikiwa mtu amepangiwa kuishi miaka 10, kila sekunde ni hatua kuelekea mwisho wa uhai wake, hivyo mwenye kulitambua hilo hawezi poteza muda kwa kufanya mambo ya upuuzi.
• Sababu ya kupatikana nidham na mpangilio: kifo kimekuwa ni sababu ya kupatikana nidhamu na mpangilio kwani bila kifo mpangilio ungeharibika, kwa mfano mtu angejisikia kumgonga mwingine na gari bila shaka wala wasi, watu wangejiachia kwenye milima, wangefikia hata kuwachezea simba sharubu zao.
• Mabadiliko ya kitabia na uadilifu: Uoga wa kifo ndio sababu ya watu kubadilika kitabia na kuwa na maadili ya kibinadamu. Kifo kimesabisha watu wenye kiburi na fahari kushuka chini na kupunguza kiburi chao, majingambo ya mali na uzuri mara tu wafikiriapo kuwa baada ya muda watakuwa ni mizoga yenye kutoa harufu na kwamba si mali, nguvu wala umashuhuri wenye kuweza kuwaokoa na kifo.
• Kupatikana elimu: Fikra ya kifo ndio imekuwa sababu ya kuchimbuka elimu mfano wa Falsafa na hata baadhi ya dini,kwani wanafalsafa walianza na kufikiria sababu ya kifo kisha wakaanza kuchambua kama tumepangiwa kufa kwanini tumepangiwa kuishi? Majibu ya swali hili yalisababisha kupatikana elimu kadhaa wa kadhaa.
Nitapenda kumalizia kwa kauli ya mtume Muhammad s.a.w: Yatumie vizuri mambo manne kabla ya manne:
1. Ujana kabla ya uzee.
2. Afya kabla ya maradhi.
3. Utajiri kamba ya ufukara.
4. Uhai kabla ya kifo.
Hakuna maana kuogopa kifo, badilika kitabia kuwa na maadili sahihi ishi kwa raha ufe kwa raha.
Tafakari!
kwa makala na visa vya hekima tembelea www.tafakuri.com