Main Title

source : abna.ir
Jumapili

19 Julai 2015

15:42:03
701451

Shambulio la kujitoa muhanga lauwa zaidi ya watu 200 katika siku ya Eid Iraq + picha

Shambulio la kujitoa mhanga lililofanywa na magaidi wa kundi Daesh kwenye soko lililofurika watu katika jimbo la mashariki la Diyala limeuwa watu zaidi ya 200 wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto katika shambulio baya kabisa katika kipindi cha muongo mmoja.

Shirika la habari la ABNA linaripoti kuwa: Shambulio la kujitoa mhanga lililofanywa na magaidi wa kundi  Daesh kwenye soko lililofurika watu katika jimbo la mashariki la Diyala limeuwa watu zaidi ya 200 wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto katika shambulio baya kabisa katika kipindi cha muongo mmoja.

Wahanga ambao wengi walikuwa ni waislamu wa dhehebu la Shia ambao  walikuwa wamekusanyika katika manunuzi ya kuadhimisha kumalizika kwa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan ambao umemalizika Ijumaa kwa Waislamu wa madhehebu ya Shia na Sunni na siku moja kabla kwa waislamu wa madhehebu ya Answari Sunna au Wahabia.

Polisi imesema lori dogo liliripuliwa kwenye soko hilo hilo lililojaa watu katika mji wa Khan Beni Saad Ijumaa ambapo mara moja sherehe ziligeuka kuwa maafa huku vipande vya miili vikiwa vimetawanyika kila mahala katika soko hilo. Maafisa wa polisi wanasema takriban watu 170 wamejeruhiwa katika shambulio hilo.

Mkazi wa Diyala Sayif Ali amekaririwa akisema "Khan Beni Saad imekuwa eneo la maafa kutokana na mripuko huo mkubwa kabisa."Ameendelea kusema kwamba "Hii ni siku ya kwanza ya Eid alfitr, mamia ya watu wameuwawa, wengi wamejeruhiwa na bado tunaendelea kutafuta miili zaidi."

Shambulio lachochea tofauti za kimadhehebu

Kundi la kigaidi la wafuasi wa kiislamu wa Answari Sunna linaloitwa Daesh limedai kuhusika na shambulio hilo katika taarifa iliowekwa kwenye mtandao wa Twitter wenye uhusiano na kundi hilo la wanamgambo.

Spika wa bunge la Iraq Salim al- Jabouri amesema Jumamosi kwamba shambulio hilo limetonesha vibaya mzozo wa madhehebu na kwamba serikali inajaribu kulidhibiti kundi hilo la kigaidi la Daesh kama linavyoiitwa kwa jina la Kiarabu lisiliyumbishe jimbo la Diyala.

Lakini ghadhabu imechemka katika jimbo hilo tete ambapo miji yake kadhaa ilitekwa na kundi hilo la kigaidi la Daesh mwaka jana. Vikosi vya kishia vya Iraq na wapiganaji wa Kikurdi wakisaidiwa na wataalamu wa vita kutoka Iran tayari wameyakombowa maeneo hayo lakini mapambano kati ya wapiganaji wa kigaidi na vikosi vya usalama vya Iraq bado yanaendelea.

Mkazi mwengine wa Diyala akizungumza kwa sharti ya kutotajwa jina kwa kuhofia kisasi amesema walikuwa wamekwenda kwenye soko hilo kufanya manunuzi na kujiadaa kwa ajili ya siku kuu hiyo ya Eid ili kuipokea kwa uchangamfu lakini furaha hiyo iligeukwa kuwa majonzi kwa kupoteza familia, marafiki na jamaa yote, kwa sababu ya serikali kushindwa kuwapatia usalama dhidi ya magaidi hao wasio na huruma.

Usalama waimarishwa maeneo mengi ya Iraq

Vikosi vya usalama vimemwagwa kwa wingi hapo Jumamosi na kuwekwa mara moja kwa vituo vipya vya ukaguzi pamoja na kuanzishwa kwa taratibu za usalama katika jimbo hilo.

Kundi hilo la wanamgambo wa kigaidi wa Answari sunna au wahabia limekuwa likihusika na mashambulizi kadhaa makubwa dhidi ya raia au vituo vya ukaguzi wakati likiwa katika harakati zao za kujitanuwa. Kundi hilo lilikuwa linadhibiti takriban theluthi moja ya Iraq na Syria eneo ambalo wamejitangazia kuwa la ukhalifa la utawala wa Kiislamu.

Hapo mwezi wa Augusti mwaka jana takriban watu 64 wameuwawa na magaidi hao katika shambulio kwenye msikiti wa Wassuni katika jimbo hilo la Diyala kwa kile wakazi wa eneo hilo wanachoamini kuwa lilikuwa ni shambulio la kulipiza kisasi dhidi ya watu wa makabila waliyokataa kutangaza utii wao kwa kundi hilo la kigaidi la Daesh la waislamu wa dhehebu la Answari sunna au Wahabia.

Mashambulizi ya anga

Serikali ya Marekani imekuwa ikitumia mabilioni kulipatia silaha na mafunzo jeshi la Iraq lakini halikufanya vizuri mwaka jana wakati vilipotimuliwa na kundi la kigaidi la Daesh waliokuwa wakiteka maeneo ya magharibi na kaskazini mwa Iraq. Muugano unaongozwa na Marekani umekuwa ukifanya mashambulizi ya anga dhidi ya maeneo yanayoshikiliwa na magaidi wa kundi hilo la Daesh nchini Iraq na Syria tokea mwaka jana lakini mashambulizi hayo yameshindwa kuzuwia kusonga mbele kwa magaidi hao kutokana na Marekani na washirika wake kutoonyesha nia thabiti ya kupambana na kundi hilo na badala yake wameonekana wakilisaidia kundi hilo kusonga mbele.

Wanamgambo hao wa kundi la kigaidi la Daesh hivi karibuni waliuteka mji wa Ramadi katika jimbo la magharibi la Iraq la Anbar na mji wa kale wa Palmyra nchini Syria ambapo kwa sasa wamekwisha rudishwa nyuma kutokana na majeshi ya kishia kuingilia kati katika kukomboa maeneo hayo wanayoishi waislamu wengi wa madhehebu ya Sunni.

Jimbo la Diyala ambalo linapakana na Iran ni jimbo pekee nchini Iraq ambapo ndege za kivita za Iran zimefanya mashambulizi ya anga dhidi ya kundi hilo mapema mwaka huu ikiwa kama hatua ya pekee ya kuwazuia magaidi hao kusonga mbele na hatimaye kuhatarisha usalama wa mipaka ya Iran. Serikali ya jimbo la Diyala imetangaza siku tatu za maombolezo.

Mwisho wa habari/ 291