Main Title

source : abna.ir
Jumatano

27 Januari 2016

19:54:50
732280

Umoja wa mataifa wataka mauaji yanayofanywa na Saudia arabia nchini Yemen yachunguzwe + Picha

Muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia mwaka jana ulizindua mashambulizi ya angani na kisha operesheni ya ardhini dhidi ya wananchi wa Yemen kwa kupinga utawala wa Rais Hadi ambaye ni mshirika wa Marekani na Saudia arabia

Shirika la habari la ABNA linaripoti kuwa: Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linapaswa kuzingatia kuundwa tume ya kimataifa ili kuchunguza madai ya ukiukaji wa haki za binaadamu unaofanywa na mashambulizi ya Saudia arabia dhidi ya wananchi wa Yemen ambayo yanaungwa mkono na Marekani, Israel, Ufaransa na Uingereza.

Hayo ni kwa mujibu wa ripoti ya kila mwaka iliyotolewa na jopo la watalaamu la Umoja wa Mataifa linalofuatilia vikwazo vya Umoja wa Mataifa.

Ripoti hiyo ya jopo la watalaamu la Umoja wa Mataifa pia inasema kuwa raia Yemen, ambalo ni taifa maskini kabisa katika ulimwengu wa Kiarabu, wanateseka kutokana na mbinu za mgogoro huo ambazo “zinajumuisha matumizi ya kunyimwa chakula kama mbinu ya vita”.

Muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia mwaka jana ulizindua mashambulizi ya angani na kisha operesheni ya ardhini dhidi ya wananchi wa Yemen wanaopinga utawala wa Rais Hadi ambaye ni mshirika wa Marekani na Saudia arabia na wanaomuunga mkono rais wa zamani, mpaka sasa majeshi ya Saudia arabia na washirika wake yakiongozwa na waatalam wa vita kutoka Uingereza na Marekani yameshindwa kusonga mbele kutokana na mapambano makali kutoka kwa wapiganaji wa Yemen wanaolinda nchi yao kuangukia kwenye mikono ya vibaraka wa Saudia arabia na Marekani, hata makundi ya kigaidi ya Al-qaida na Daesh ambayo yanapigana kwa kulipwa na Saudia arabia yameshindwa kusonga mbele nchini Yemen, hivyo Saudia arabia imejikuta ikipata hasara katika uwanja wa vita na badala yake imeamua kumalizia hasira zake kwa kushambulia nyumba na miundo mbinu ya Yemen.

Zaidi ya watu 16,000 wameuawa na wengine wengi kujeruhiwa vibaya na zaidi ya asilimia 80 ya idadi ya watu nchini Yemen wanahitaji kwa dharura chakula, maji, makazi na msaada mwingine , kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa. Juhudi za kufanyika mazungumzo ya amani chini ya upatanisho wa Umoja wa Mataifa yamegonga mwamba kufikia sasa.

Umoja wa Mataifa umeuzungumzia kwa kiasi kikubwa mzozo huo na athari zake katika siku za karibuni. Mapema mwezi huu, serikali ya Yemen ilimfukuza kwa muda mfupi mwakilishi wa haki za binaadamu nchini humo baada ya ofisi ya haki za binaadamu ya Umoja wa Mataifa kusema ilipokea madai kuwa majeshi ya muungano unaoongozwa na Saudi Arabia walitumia mabomu ya sumu katika mashambulizi yake.

Katika wakati huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon alielezea wasiwasi wake mkubwa kuhusu “kuongezeka” kwa mashambulizi ya angani ya muungano huo unaoungwa mkono na Marekani na akaonya kuwa ripoti za matumizi ya mabomu ya sumu katika maeneo yenye watu wengi kunaweza kuwa ni uhalifu wa kivita.

Ripoti hiyo mpya inasema kuwa katika baadhi ya matukio, iligundua kuwa muungano huo uliwalenga raia katika mashambulizi hayo kwa mpangilio. Jopo hilo linasema liliratibu mashambulizi 119, yanayohusiana na ukiukaji wa sheria ya kimataifa ya kiutu, huku mashambulizi mengi yakiwalenga raia wasio na hatia.

Aidha kuna matukio matatu yanayodaiwa kuwa ya raia waliokuwa wakitoroka mabomu yaliyokuwa yakiangushwa katika makaazi yao na kisha wakafuatwa na kupigwa risasi na helikopta za Saudia arabia . Jopo hilo halikuruhusiwa kwenda Yemen, kwa hivyo lilitegemea picha za satelaiti na vyanzo vingine katika uchunguzi wake.

Ripoti hiyo pia inasema muungano huo wa kijeshi unaoongozwa na Saudia umetekeleza jukumu la moja kwa moja katika ueneaji wa silaha nchini Yemen kwa kuyapa silaha makundi ya kigaidi ikiwemo Al-qaida na Daesh yanayoshiriki katika vita bila kuchukua hatua za kuhakikisha uwajibikaji na kuhifadhiwa silaha hizo katika njia iliyo bora.

Mwisho wa habari/ 291