Main Title

source : abna.ir
Jumamosi

26 Novemba 2016

19:30:37
794514

Shujaa Fidel Castro afariki dunia + Picha

Shujaa, mwana mapinduzi na Kiongozi maarufu wa Cuba Fidel Castro amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 90. Mwanamapinduzi huyo ameacha historia kubwa ya kupambana na udikteta na kupigania haki, ambapo serikali ya Marekani ilifanya majaribio mengi ya kumuua lakini haikufanikiwa na badala yake wakaiadhibu Cuba kwa kuiwekea vikwazo serikali ya Cuba na kuzuia mali za nchi hiyo zilizokuwa katika mabenki lakini pia haikukubali kuisujudia Marekani.

Shirika la habari la ABNA linaripoti kuwa: Shujaa, mwana mapinduzi na Kiongozi maarufu wa Cuba Fidel Castro amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 90. Mwanamapinduzi huyo ameacha historia kubwa ya kupambana na udikteta na kupigania haki, ambapo serikali ya Marekani ilifanya majaribio mengi ya kumuua lakini haikufanikiwa na badala yake wakaiadhibu Cuba kwa kuiwekea vikwazo serikali ya Cuba na kuzuia mali za nchi hiyo zilizokuwa katika mabenki lakini pia haikukubali kuisujudia Marekani.

Kifo chake kimetangazwa na mdogo wake, rais wa sasa wa Cuba Raul Castro. ''Kamanda wa mapinduzi ya Cuba, Fidel Castro Ruz, amefariki dunia saa nne na dakika ishirini na tisa usiku'', amesema Rais Raul Castro kupitia televisheni ya taifa, bila kutaja chanzo cha kifo hicho.

Fidel Castro, miongoni mwa watu muhimu katika karne ya 20, alijenga taifa la kikomunisti jirani na Marekani, akihimili njama za Marekani za miaka 50 za nchi hiyo kutaka kuiangusha serikali yake. Aliendelea kushikilia sera zake za kikomunisti hata baada ya kusambaratika kwa iliyokuwa Umoja wa Kisovieti, ambayo ilikuwa chanzo kikuu cha msaada kwa Cuba, ambayo ilikuwa chini ya vikwazo vikali vya kidhalimu vya Marekani.

Aliingia madarakani mwaka 1959 baada ya kuiangusha serikali ya dikteta Fulgencio Batista, aliyekuwa akiungwa mkono na utawala dhalimu wa Marekani, na alibakia madarakani hadi mwaka 2008 alipokabidhi madaraka kwa mdogo wake, Raul.

Kiongozi wa aina yake

Fidel Castro alijulikana kwa kutoa hotuba ndefu zenye hamasa na hekima, za masaa matano hadi saba bila kupumzika. Makala zake katika gazeti la chama chake cha kikomunisti ''Granma'' ziliishambulia Marekani bila kuchoka, akilishutumu Marekani kwa  kuiba na kunyakuwa raslimali nyingi za dunia.

Shujaa huyu Alizaliwa mwaka 1926 katika maeneo ya vijijini Mashariki mwa Cuba, kwenye familia iliyokuwa na uwezo mzuri kifedha. Wakati wa ujana wake alifanya kazi kama mwanasheria katika mji mkuu wa Cuba, Havana, mara nyingi akiwa wakili wa watu masikini.

Safari yake ya siasa aliinza akiwa mdogo. Akiwa na umri wa miaka 26 aligombea ubunge, lakini aliambulia patupu wakati Fulgencio Batista alipoingia madarakani kupitia mapinduzi ya kijeshi. Castro akaazimia kumuondoa madarakani Batista kwa njia yoyote ile, na akaunda ushirika na watu wenye mtazamo wa kimapinduzi kama yeye, akiwemo shujaa Ernesto ''Che'' Guevara.

Tarehe 1 Januari, 1959, Fulgencio Batista alilemewa nguvu na kuikimbia nchi. Castro akaingia madarakani, akichukuliwa na wacuba wengi kama mkombozi.

Castro alikuwa Cuba, na Cuba ilikuwa Castro

Seraza kisoshalisti za Castro zilimfanya afarakane na Marekani na kuegemea upande wa iliyokuwa Umoja wa Kisovieti -USSR, na nchi zilizokuwa chini ya ushawishi wake, ikiwemo Ujerumani Mashariki wakati huo. USSR iliendelea kuiunga mkono kijeshi Cuba, na mwaka 1962 iliweka katika nchi hiyo makombora ya nyuklia ya masafa ya kati, hali iliyozusha mvutano mkubwa na kuisogeza dunia karibu kabisa na vita vya kinyuklia. Baada ya kusambaratika kwa Umoja wa Kisovieti mwanzoni mwa miaka ya 1990, Cuba ilipitia kipindi kigumu kabisa kiuchumi baada ya Marekani kuiwekea vikwazo vya kidhalimu kwa uadui binafsi na kuisingizia serikali ya Cuba kuwa inadhamini magaidi, na hii ndio sera ya Marekani inayotumika mpaka sasa, ambapo Korea kaskazin, Iran na Syria pia zimewekewa vikwazo vya kidhalimu na Marekani.

Cuba inajulikana kama nchi yenye mfumo bora kabisa wa elimu na afya katika Ukanda wa Karibeani, kutokana na uwekezaji mkubwa wa Castro katika sekta hizo. Lakini, kiongozi huyo hakuvumilia upinzani, na wakosoaji wengi waliishia jela.

Maja Liebing, afisa wa shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International, kitengo cha Cuba, anasema Castro atakumbukwa kama mtu aliyewatia kizuizini mamia ya wakosoaji, hata kwa sababu ndogo tu kama kuandamana kwa amani. Mamia kwa maelfu ya wacuba waliihama nchi yao kutokana msimamo mkali wa Castro kuelekea upinzani na ukosoiaji wa kisiasa.

Mungu amlaze pema Shujaa huyu

Hatimaye, kutokana na uzee na afya yake iliyokuwa ikizidi kudhoofika, Fidel Castro aling'atuka madarakani mwaka 2006. Mwaka 2008, mdogo wake Raul alichukua rasmi madaraka, akimaliza miaka 49 ya kaka yake madarakani. Castro alikuwa kiongozi aliyetawala muda mrefu zaidi katika karne ya 20.

Raul alianza taratibu kuifungua milango ya nchi. Serikali yake iliwafungua wafungwa 30 wa kisiasa Januari mwaka 2015, wakati Marekani ilipotangaza kuilegezea vikwazo vyake vya kidhalimu kwa Cuba katika masuala ya usafiri na biashara haya yalijiri katika utawala wa Obama.

Castro, ambaye aliwahi kusema, ''usoshalisti au kifo'', hakusema mengi wakati nchi yake ilipopiga hatua kurejesha uhusiano na Marekani ambayo imekuwa ikifanya juhudi zake zote kuhakikisha Cuba inaangamia.

Akizungumza katika mkutano mkuu wa chama cha kikomunisti mwezi Aprili mwaka huu wa 2016, Fidel Csstro alisema, ''Hivi karibuni nitatimiza umri wa miaka 90, na punde nitafuata njia ya wengine''. Aliendelea kusema kuwa kila mtu anao mwisho wake, lakini ''maadili ya kikomunisti ya Cuba yatabakia kama ushahidi katika dunia hii, kwamba watu wakifanya kazi kwa bidii na kwa uadilifu, wanaweza wakafanikiwa kutenda mema kwa binadamu, kiuchumi na kiutamaduni, na kuyafikia hayo, lazima kupigana na dhulma bila kusalimu amri''.

Mwisho wa habari/ 291