Main Title

source : Pars Today
Jumatano

26 Juni 2019

09:09:13
955238

Misimamo ya kimasharti ya troika ya Ulaya kuhusu JCPOA

Huku muda uliowekwa na Iran wa kuongeza kiwango cha kutochunga ahadi zake ndani ya mapatano ya nyuklia ya JCPOA kutokana na upande wa pili wa mapatano hayo kutotekeleza ...

(ABNA24.com) Huku muda uliowekwa na Iran wa kuongeza kiwango cha kutochunga ahadi zake ndani ya mapatano ya nyuklia ya JCPOA kutokana na upande wa pili wa mapatano hayo kutotekeleza kabisa ahadi zao ukikaribia, troika ya Ulaya yaani nchi tatu za Ujerumani, Ufaransa na Uingereza zimeanzisha harakati za kidiplomasia na kipropaganda za kujaribu kuizuia Iran isichukue hatua zaidi za kupunguza utekelezaji wa ahadi zake.

Nchi hizo tatu za Ulaya zimetoa taarifa ya pamoja na sambamba na kuelezea wasiwasi wao kuhusu kuongezeka mivutano na mizozo katika eneo la Asia Magharibi, zimehimiza kutekelezwa kikamilifu vipengee vya mapatano ya JCPOA. Taarifa yao hiyo imesema kwamba, kwa kuzingatia kuwa karibuni hivi kutaitishwa kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kitakachozungumzia azimio nambari 2231 la mapatano ya JCPOA; Ufaransa, Ujerumani na Uingereza zinahimiza kutekelezwa kikamilifu vipengee vya mapatano hayo. Sehemu nyingine ya taarifa hiyo ya troika ya Ulaya inasema: Tunaamini kwamba kutekelezwa kikamilifu makubaliano hayo kutapounguza mizozo na wasiwasi katika eneo hilo na kutazuia kuenea silaha za nyuklia ulimwenguni. Nchi hizo tatu za Ulaya zimedai kuwa, zinataka kutekelezwa na kuheshimiwa kikamilifu azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kuzitaka pande nyingine za makubaliano hayo kuwa na msimamo kama huo na zijiepushe kuyadhoofisha mapatano hayo ambayo ni nguzo kuu ya mfumo wa kuzuia kuenea silaha za nyuklia na kuleta usalama kwa wote.

Madai yaliyotolewa na nchi tatu za Ulaya za Ufaransa, Ujerumani na Uingereza yanakinzana na vitendo vyao kuhusu utekelezaji wa vipengee vya JCPOA. Baada ya Marekani kujitoa katika mapatano hayo tarehe 8 Mei 2018, wanachama wa barani Ulaya waliobakia kwenye mapatano hayo walitangaza kuwa watachukua hatua za kukabiliana na athari hasi za vikwazo vya upande mmoja vya Marekani dhidi ya Iran na wataendelea kufanya biashara na Tehran. Vile vile waliahidi kuanzisha mfumo maalumu wa kifedha baina ya Ulaya na Iran unaojulikana kwa jina la INSTEX ili kukwepa vikwazo vya kifedha vya Marekani. Hata hivyo hadi leo hii nchi hizo hazijaanza kutekeleza mpango huo licha ya kwamba zinadai kuwa zinaheshimu mapatano ya JCPOA na licha ya Marekani kuiwekea vikwazo kila leo Iran, na wakati huo huo zinaitaka Tehran isichukue hatua yoyote ya kukabiliana na uadui wa Marekani.

Tab'an Iran si nchi ambayo inaweza kukaa vivi hivi bila ya kujibu uadui inaofanyiwa. Ndio maana katika kujibu kitendo cha nchi za Ulaya cha kudharau kutekeleza ahadi zao, Iran kuanzia Jumatano ya tarehe 8 Mei 2019 na baada ya kuvumilia mwaka mzima, ilitoa tamko la kupunguza kiwango cha ahadi zake ndani ya mapatano ya JCPOA tena kwa mujibu wa sheria na kwa mujibu wa vipengee vya 26 na 36 vya mapatano hayo ambavyo vinaipa Iran haki hiyo. Katika taarifa yake ya tarehe 8 Mei 2019, Iran ilizipa nchi za Ulaya muda wa siku 60 kuhakikisha zinatekeleza ahadi zao vinginevyo itachukua hatua kubwa zaidi za kutotekeleza ahadi zake ndani ya JCPOA.

Licha ya kwamba hivi sasa takriban siku 50 zimeshapita tangu kutolewa makataa hayo na Iran, lakini bado nchi za Ulaya hazijachukua hatua za maana za kutekeleza kivitendo ahadi zao za kuanzisha mfumo wa mabadilishano ya fedha wa INSTEX. Ukweli ni kwamba nchi za Ulaya zinataka mapatano ya JCPOA yaheshimiwe na Iran tu na haziko tayari kugharamia chochote katika utekelezaji wa mapatano hayo. Ni jambo lililo wazi kuwa jambo hilo haliingii akilini hasa kwa kutilia maanani kuwa kuitaka Iran iheshimu peke yake mapatano hayo ni kinyume cha sheria na hakiendani na vipengee vya JCPOA. Cha kushangaza ni kuwa, nchi hizo za Ulaya hata zinatumia lugha ya vitisho kuilazimisha Iran iheshimu peke yake mapatano hayo. Hivi karibuni msemaji wa serikali ya Uingereza alisema: Sisi tunashikiriana na waitifaki wetu kuyalinda mapatano ya JCPOA; lakini kama Tehran itakataa kushirikiana nasi, sisi pia tutaanza kuchunguza hatua nyingine za kuchukua.

Nchi za Ulaya zinaonesha wazi kwamba kutamka kwao kwa maneno tu kuwa zinaheshimu mapatano ya JCPOA ni muhimu zaidi kuliko hata hatua za Iran za kutekeleza kivitendo vipengee vyote vya makubaliano hayo. Abbas Araqchi, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alisema wakati alipoonana na  Andrew Morrison, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza kwamba, inasikitisha kuona kuwa hakuna mlingano wowote wa utekelezaji wa majukumu baina yetu ndani ya JCPOA, hivyo Tehran haioni haja ya kuendelea kuheshimu peke yake vipengee vya mapatano hayo.

Ni jambo lililo wazi kwamba lawama za madhara ya kupunguza Iran ahadi zake ndani ya JCPOA zitaliendea kundi la 4+1 zilizobakia kwenye mapatano hayo hasa nchi za Ulaya ambazo hadi leo hii zinakwepa kutekeleza ahadi zao; tofauti na Iran ambayo ripoti 14 za Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA zimethibitisha kuwa imetekeleza kikamilifu ahadi zake zote.




/129