Main Title

source : Pars Today
Jumapili

30 Juni 2019

10:35:04
956350

Malengo ya safari ya mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia nchini Korea Kusini

Mohammad bin Salman, mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia, Jumatano tarehe 26 Juni aliwasili Seoul, mji mkuu wa Korea Kusini na kufanya mazungumzo ya ana kwa ana na Rais Moon Jae-in wa nchi hiyo.

(ABNA24.com) Mohammad bin Salman, mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia, Jumatano tarehe 26 Juni aliwasili Seoul, mji mkuu wa Korea Kusini na kufanya mazungumzo ya ana kwa ana na Rais Moon Jae-in wa nchi hiyo.

Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, ziara hiyo ya Bin Salman huko Korea Kusini inaweza kutathminiwa katika chanjaa kadhaa.

Kwanza ni kwamba hiyo ni ziara ya kwanza kabisa ya Bin Salman nchini Korea Kusini tangu mwaka 1998.

Pili ni kwamba hiyo ni safari ya kwanza kabisa ya mrithi huyo wa kiti cha ufalme wa Saudia tangu baada ya kutolewa ripoti ya ripota maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu kuhusika kwake katika maujai ya kikatili ya mwandishi wa habari mkosoaji, Jamal Khashoggi, katika ubalozi mdogo wa Saudi Arabia mjini Istanbul, Uturuki. Hivyo wachambuzi hao wa mambo wanasema, ziara hiyo ina umuhimu mkubwa kwa Bin Salman kwani ana hamu ya kuonesha kuwa ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa haijamuathiri kivyovyote vile.

Tatu ni kwamba Mohammad bin Salman ameelekea Korea Kusini katika hali ambayo ameshindwa kutembelea nchi yoyote ya Ulaya na Marekani katika kipindi cha miezi tisa iliyopita kutokana na kashfa ya mauaji ya kinyama ya Jamal Khashoggi. Katika kipindi cha miezi tisa iliyopita, Bin Salman ametembelea nchi kadhaa za Kiarabu pamoja na China, India na Pakistan, lakini ameshindwa kutembelea nchi za Ulaya na Marekani. Inaonekana wazi kuwa kadhia ya Khashoggi imetoa pigo kubwa kwa mrithi huyo wa kiti cha ufalme wa Saudia na malalamiko makubwa ya mashirika ya haki za binadamu na wananchi za nchi za Magharibi yanamtia woga wa kuzitembelea nchi hizo.

Nne ni kwamba Mohammad bin Salman anafuatilia masuala ya muhimu ya kiuchumi huko Korea Kusini. Inavyoonekana ni kuwa mrithi huyo wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia anafanya juhudi za kuzitumia nchi za mashariki mwa Asia kama kigezo cha kiuchumi kwa ajili ya nchi yake. Wakati huo huo Bin Salman anataka kustafidi na uwezo wa kiuchumi wa nchi kama China, Japan na Korea Kusini hivyo anajaribu kuzishawishi nchi hizo ziwezekeze huko Saudi Arabia.

Itakumbukwa kuwa shirika kubwa zaidi la mafuta la Saudia (ARAMCO) lina vitega uchumi vingi huko Korea Kusini. Shirika hilo pia hivi sasa ndilo lenye hisa kubwa zaidi katika kampuni ya tatu kwa ukubwa ya mafuta nchini Korea Kusini yaani asilimia 63.41 ya hisa za kampuni ya uchimbaji mafuta ya S-Oil ya Korea Kusini, ni ya Saudi Arabia. 

Amin H. Nasser, mkurugenzi mtendaji wa shirika la mafuta la Saudia, ARAMCO amesema kuwa, Mohammad bin Salman atafungua zoezi la kulipanua shirika la mafuta la S-Oil katika mradi ambao utagharimu dola bilioni 4.2 za Kimarekani.

Ni jambo lililo wazi kwamba ziara hiyo ya Bin Salman huko Korea Kusini ina mfungamano na hati ya 2030 ya Saudi Arabia na inatabiriwa kuwa katika ziara hiyo, mrithi huyo wa kiti cha ufalme wa Saudia atazungumza na wakuu wa mashirika mbalimbali ya Korea Kusini kuhusu ushirikiano wa nchi hiyo na Saudi Arabia katika ufanikishaji wa hati hiyo.

Ukweli ni kwamba Korea Kusini inaingalia Saudi Arabia kwa jicho la kiuchumi zaidi na haina malengo ya kisiasa. Korea Kusini ni mnunuzi mkubwa wa mafuta ya Saudia kiasi kwamba katika kipindi cha miezi minne ya mwanzoni mwa mwaka huu wa 2019, imenunua mapipa milioni 101.5 kutoka kwa Saudi Arabia. Tab'an kiwango hicho kimepungua kwa asilimia 2.7 ikilinganishwa na mwaka jana. Kwa mujibu wa televisheni ya Euro News, mwaka 2018, Korea Kusini ilinunua mapipa milioni 323,017 ya mafuta ghafi kutoka kwa utawala wa kifalme wa Saudia ambayo ilikuwa ni sawa na mapipa 885.408 kwa siku. 

Mbali na jambo hilo, Korea Kusini ina hamu ya kushiriki katika ujenzi wa viwanda vya nyuklia nchini Saudi Arabia. Ndio maana mwezi Julai mwaka jana 2018, shirika la kuzalisha umeme la Korea Electric liliwasilisha rasmi ombi lake la kutaka lipewe zabuni ya kujenga vinu vya nyuklia nchini Saudi Arabia.


/129