Main Title

source : Pars Today
Jumatatu

1 Julai 2019

02:22:07
956448

Sababu ya jeshi la Uturuki kushambulia maeneo ya jeshi la Syria

Wizara ya Ulinzi ya Uturuki imetangaza sababu ya kuyalenga maeneo ya jeshi la Syria.

(ABNA24.com) Taarifa iliyotolewa Ijumaa na Wizara ya Ulinzi ya Uturuki inasema kuwa, jeshi la Uturuki liliyashambulia baadhi ya maeneo ya jeshi la Syria ndani ya ardhi ya nchi hiyo ya Kiarabu. Katika taarifa hiyo Wizara ya Ulinzi ya Uturuki imedai kwamba hatua hiyo ilichukuliwa kama jibu dhidi ya shambulizi lililotekelezwa katika kituo kimoja cha usimamizi cha Uturuki katika mkoa wa Idlib nchini Syria. Hatua ya jeshi la Uturuki kushambulia maeneo ya jeshi la Syria imejiri katika hali ambayo, serikali ya Ankara imeyakalia kwa mabavu maeneo kadhaa ya Syria kinyume cha sheria. Serikali ya Uturuki kwa kushirikiana na Marekani na baadhi ya serikali za Ulaya na bila idhidi ya serikali halali ya Damascus, ilivamia na kukalia kwa mabavu baadhi ya ardhi ya Syria tangu mwaka 2011. Katika mazingira hayo, Ankara inajaribu kukabiliana na jeshi la Syria, ili iweze kufikia malengo yake machafu ndani ya nchi hiyo.

Serikali ya Uturuki imeweka kambi za majeshi yake nchini Syria bila idhini ya serikali ya Damascus. Ni kwa ajili hiyo ndio maana serikali halali ya Syria tangu mwanzo wa kuanza operesheni za Uturuki ndani ya ardhi ya nchi hiyo sambamba na kulaani vikali hatua hiyo, ikatangaza kuwa ni ishara ya wazi ya ukiukaji wa haki yake ya kujitawala. Katika uwanja huo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria imetangaza kwamba: "Lengo la Uturuki sio kupambana na makundi ya kigaidi likiwemo kundi la Daesh (ISIS), bali Ankara inakusudia kuyaweka makundi mengine ya kigaidi mahala pa Daesh." Uturuki imetangaza sababu ya kushambulia jeshi la Syria katika hali ambayo kabla ya hapo viongozi wa Ankara walikuwa wamesema kuwa hawakuwa na tamaa yoyote na ardhi za Syria. Kwa mfano, Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki amewahi kuashiria mara kadhaa suala hilo. Pamoja na hayo, tajriba inaonyesha kwamba licha ya rais huyo kutoa matamshi kama hayo, lakini huwa hafungamani na ahadi zake na inawezekana pia msimamo wa rais huyo ukawa umebadilika kuzihusu nchi jirani. Tokea viongozi viongozi wa chama cha Uadilifu na Ustawi waliokuwa wakisisitiza juu ya sera ya 'mizozo sifuri na majirani' watwae madaraka nchini Uturuki, nchi hiyo imeingia katika vita na nchi mbili jirani. Harakati za kijeshi za Uturuki katika nchi jirani zimeshika kasi ambapo mbali na wananchi kuzipinga, zimekuwa zikipingwa pia na viongozi wa vyama vya kisiasa nchini humo.

Akthari ya weledi wa masuala ya kisiasa na wanafikra wa Uturuki kuhusu masuala ya kieneo wanaamini kwamba, siasa za uvamizi dhidi ya ardhi za Syria zinazotekelezwa na jeshi la Uturuki ni za kiuadui na zinakinzana wazi na maslahi ya kitaifa ya Uturuki. Kwa mfano tu Turcker Arturck, askari mstaafu wa jeshi la wanamaji na mtaalamu wa masuala ya kijeshi wa Uturuki anasema: "Siasa za serikali ya Uturuki kuihusu Syria zimekuwa na makosa makubwa na ni lazima serikali ya Ankara izitazame upya. Ukweli ni kwamba badala ya Uturuki kuwa na uhusiano mzuri na nchi za eneo hususan Syria, daima imekuwa ikielekea upande wa kuibua mzozo katika uhusiano na nchi za eneo." Kiujumla tunaweza kusema kuwa, wakati Uturuki ilipoanza kutekeleza siasa za kutaka kupenya kijografia katika eneo kwa lengo la kutaka kuhuisha kipindi cha utawala wa Othmania kwa madhumuni ya kuingia katika ushindani na nchi za eneo la Asia Magharibi, haikudhania kwamba njia hiyo ingekuwa ngumu kama ilivyo sasa. Na hasa tukitilia maanani kwamba kuendelea kuimarika serikali ya nchi mbili za Iraq na Syria kunahatarisha uwepo haramu wa askari wa Uturuki katika ardhi ya nchi hizo.




/129