Main Title

source : Pars Today
Jumamosi

13 Julai 2019

08:15:39
960458

2019, mwaka wa kunyongwa watu zaidi nchini Saudi Arabia

Vyombo vya habari vimeripoti kuwa kesi za kunyongwa watu nchini Saudi Arabia zimeongezeka mara mbili katika nusu ya kwanza ya mwaka huu wa 2019.

(ABNA24.com) Vyombo vya habari vimeripoti kuwa kesi za kunyongwa watu nchini Saudi Arabia zimeongezeka mara mbili katika nusu ya kwanza ya mwaka huu wa 2019.

Mwezi Aprili mwaka jana wa 2018 wakati Muhammad bin Salman alipoteuliwa na baba yake kuwa mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia aliahidi kuwa, atapunguza visa vya kunyonga watu nchini humo. Hata hivyo ahadi hiyo imeishia kwenye maneno tu na kivitendo visa vya kunyongwa watu vimeongezeka zaidi nchini humo. Kuhusu suala hilo Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Ulaya limetangaza kuwa: Idadi ya watu walionyongwa nchini Saudi Arabia katika kipindi cha miezi sita iliyopita ndiyo kubwa zaidi kuwahi kusajiliwa katika kipindi cha miaka mitano ya hivi karibuni. Miezi sita ya mwanzo ya mwaka 2018 watu 55 walinyongwa Saudia, na idadi hiyo katika miezi sita ya mwanzoni mwa mwaka huu wa 2019 imefikia watu 122 yaani imeongezeka na kuwa zaidi ya mara mbili ya mwaka wa kabla yake.

Jambo lenye umuhimu zaidi ni kuwa, karibu nusu ya watu ho walihukumiwa kifo kwa sababu na makosa ya kisiasa yaliyoarifishwa kwa mujibu wa sheria ya eti kupambana na ugaidi. Kwa mujibu wa sheria hiyo, ukosoaji wa aina yoyote dhidi ya muundo wa utawala wa kifalme wa Saudi Arabia unatambuliwa kuwa ni kosa la jinai na adhabu yake ni ama kuuawa au kifungo cha muda mrefu jela. Ni vyema pia kueleza hapa kwamba, idadi kubwa ya wafungwa wa kisiasa nchini Saudi Arabia ni Waislamu wa madhehebu ya Shia, na kwa msingi huo huo Waislamu wa madhehebu hiyo ndio wanaounda idadi kubwa zaidi ya Wasaudia wanaohukumiwa kifo na kuuawa na mahakama za nchi hiyo. Kwa mfano katika siku moja tu yaani tarehe 23 Aprili watu 37 walinyongwa nchini Saudi Arabia na wengi wao ni wale waliohukumiwa kifo kwa kosa la kushiriki katika maandamano ya Waislamu wa madhehebu ya Shia dhidi ya dhulma za serikali ya Saudi Arabia. Raia wa kigeni pia hawakusalimika na upanga wa utawala wa Saudia. Katika kipindi cha miezi sita iliyopita raia 57 wa kigeni waliuawa kwa kukatwa vichwa nchini humo.  

Suala jingine linalopaswa kuashiriwa ni kwamba, hukumu za kukatwa vichwa watu nchini Saudi Arabia zimekuwa zikitolewa bila ya kufikishwa katika mahakama za kiadilifu. Aghlabu ya watu waliokatwa vichwa au wanaosubiri kukatwa vichwa hawakujulishwa hata makosa na tuhuma zilizokuwa zikiwakabili, na mahakama za Saudia hazikuonesha ushahidi wa aina yoyote wa kuthibitisha makosa na tuhuma hizo. Wahanga hao wamekuwa wakiuawa kwa tuhuma za kubuni tu au tuhuma kama eti kutishia usalama wa raia. Hii ina maana kwamba, mfumo wa mahakama za Saudia unaathiriwa na siasa za Aal Saud hasa kwa kutilia maanani kwamba, nchi hiyo haina mfumo wa mihimili mitatu mikuu ya dola.

Ni kwa kutilia maanani mienendo hiyo ya watawala wa Saudia ndipo jarida la Newsweek likaandika kuwa: "Sera ya sasa ya kujikita zaidi kwa wapinzani wa kisiasa inaonesha kuwa, Saudi Arabia imeingia katika kipindi cha ukandamizaji angamizi." Maneno haya yanapata nguvu zaidi kwa kutilia maanani kwamba, watu 714 wameuwa kwa kukatwa vichwa tangu Salman bin Abdul Aziz alipokalia kiti cha ufalme wa Saudia.

Suala jingine ni kwamba, tawala za nchi za Magharibi ambazo zilishupalia na kuvalia njunga mauaji ya mwandishi habari na mkosoaji wa utawala wa kifalme wa Saudia, Jamal Khashoggi, hazijatoa hata taarifa madhubuti ya kulaani mauaji ya idadi kubwa ya watu wanaohukumiwa katika mahakama za kimaonyesho nchini humo. Msimamo huu unawashajiisha viongozi wa Riyadh hususan mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia, Muhammad bin Salman kuendeleza ukatili na mauaji ya raia kwa kutumia visingizio visivyo na msingi.      





/129