Main Title

source : Pars Today
Jumanne

30 Julai 2019

10:00:28
965847

Kupigwa marufuku shughuli za Harakati ya Kiislamu ya Nigeria na taathira zake

Wakati Waislamu wa Nigeria wakiendeleza jitihada za kuhakikisha kwamba kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya nchi hiyo, Sheikh Ibrahim Zakzaky anaachiwa huru, Rais wa nchi hiyo amepiga marufuku shughuli zote za harakati hiyo.

(ABNA24.com) Wakati Waislamu wa Nigeria wakiendeleza jitihada za kuhakikisha kwamba kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya nchi hiyo, Sheikh Ibrahim Zakzaky anaachiwa huru, Rais wa nchi hiyo amepiga marufuku shughuli zote za harakati hiyo.

Ofisi ya Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria imetangaza kuwa shughuli zote za Harakati ya Kiislamu inayoongozwa na Sheikh Ibrahim Zakzaky zimepigwa marufuku. Tangazo hilo limetolewa baada ya miaka kadhaa ya ukandamizaji mkubwa na mashinikizo ya kisiasa na kijamii ya vyombo vya usalama vya Nigeria dhidi ya Waislamu hususan wafuasi wa Sheikh Zakzaky ambaye alikamatwa na kuwekwa korokoroni tangu mwaka 2015. Kutiwa nguvuni mwanazuoni huyo wa Kiislamu ulikuwa mwanzo wa kuongezeka mashinikizo dhidi ya Waislamu, na kiongozi huyo angali anashikiliwa gerezani kwa kipindi cha karibu miaka minne sasa licha ya Mahakama Kuu ya Nigeria kuiagiza serikali imwachie huru Disemba mwaka 2016. Suala hilo limezusha hasira baina ya Waislamu wa Nigeria ambao wamekuwa wakiandamana wakitaka serikali ya Abuja imwachie huru kiongozi wao. Vyombo vya dola vimekuwa vikikabiliana kwa mkono wa chuma na maandamano ya amani ya Waislamu hao kwa kadiri kwamba, mamia ya waandamanaji hao wameuawa kwa kupigwa risasi au wakiwa katika mikusanyiko ya kidini kama vikao na majlisi za kukumbuka mauaji ya mjukuu wa Mtume Muhammad (saw) katika siku ya Ashura.

Habari iliyotangazwa wiki za hivi karibuni ya kuzidi maradhi ya Sheikh Ibrahim Zakzaky na kudhoofika hali yake ya kimwili baada ya kulishwa sumu ndani ya jela ya serikali ya Nigeria imezidisha hasira za Waislamu wa nchi hiyo. Waislamu hao na jumuiya mbalimbali za kutetea haki za binadamu wametoa wito wa kuachiwa huru mara moja mwanazuoni huyo na mkewe na kuruhusiwa kupewa matibabu nje ya nchi. Serikali ya Buhari inaendelea kupuuza wito huo na kuendeleza mauaji dhidi ya waandamanaji.

Uchunguzi wa mwenendo wa kisiasa nchini Nigeria unaonesha kuwa, sababu kuu ya misimmo ya sasa ya serikali ya Nigeria dhidi ya Waislamu hususan wafuasi wa madhehebu ya Ahlul Bait ni ushawishi wa Marekani, Israel na Saudi Arabia katika serikali ya Abuja. Kuongezeka kwa mvuto wa kiroho na kimaanawi wa Waislamu hususan wa madhehebu ya Ahlubaiti wa Mtume (saw) nchini Nigeria na katika nchi nyingi za Afrika sambamba na utajiri mkubwa wa nishati na maliasili nyingine vimezifanya baadhi ya nchi kama Marekani, Saudi Arabia na utawala wa Kizayuni wa Israel zizidishe uhusiano wao na serikali ya Abuja na kuweza kutekeleza siasa zao za kishetani na kukandamiza harakati na mwamko huo wa Kiislamu. Siasa hizo zinatekelezwa kupitia njia ya kuiuzia silaha Nigeria au misaada ya kifedha.

Sheikh Adam Soko ambaye ni mjumbe wa ngazi ya juu wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria anasema: "Serikali ya Nigeria iko chini ya satua na ushawishi wa Marekani, Israel na Saudi Arabia na tawala hizo zote zinasuka njama na hila dhidi ya Waislamu hususan wafuasi wa madhehebu ya Ahlul Bait."

Haya yote ni licha ya kwamba Waislamu hususan wale wa madhehebu ya Shia wamekuwa wakiishi kwa amani na raia wa dini na madhehebu nyingine nchini Nigeria na kwa kuheshimu sheria za nchi. Shua'ib Mussa ambaye ni mhadhiri wa chuo kikuu nchini Nigeria anasema: "Marekani na waitifaki wake wanafanya jitihada za kufuta uhuru wa kidini unaodhaminiwa na katiba ya Nigeria na hatimaye kuzusha hitilafu baina ya madhehebu na dini tofauti nchini humo."

Serikali ya Nigeria imezidisha mashinikizo na mbinyo dhidi ya Waislamu hususan wa madhehebu ya Shia wakati nchi hiyo inasumbuliwa na changamoto nyingi za ndani na nje. Mashambulizi ya kundi la kigaidi la Boko Haram yamevuruga amani na usalama katika maeneo mbalimbali ya Nigeria hususan kaskazini mwa nchi hiyo na kuwalazimisha mamilioni ya watu kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi. Nigeria pia inasumbuliwa na umaskini mkubwa unaoathiri maisha ya watu wa kawaida, ukosefu wa ajira na usalama mdogo katika maeneo yenye utajiri wa mafuta ya kusini mwa nchi hiyo.

Kwa kuzingatia hayo yote inaonekana kuwa, hatua ya serikali ya Rais Muhammadu Buhari ya kupiga marufuku shughuli za Harakati ya Kiislamu nchini humo inaweza kuzidisha matatizo ya kijamii na kiusalama na kupanua ufa na migawanyiko ndani ya nchi hiyo yenye jamii kubwa zaidi ya watu barani Afrika.




/129