Main Title

source : ParsToday
Jumamosi

4 Januari 2020

08:24:06
999147

Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran limetoa tamko maalumu kufuatia jinai ya Marekani ya kumuua shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH. Taarifa hiyo ya jana Ijumaa ilitolewa baada ya kikao cha dharura cha baraza hilo ambacho kilichunguza pembe mbalimbali za tukio hilo la kuchukua maamuzi yanayofaa.

(ABNA24.com) Katika tamko lake hilo, Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran limesema:

Marekani itambue kuwa, shambulio lake la kijinai ni kosa kubwa mno la kiistratijia lililofanywa na nchi hiyo katika eneo hili la Asia Magharibi na kwamba Washington haitotoka vivi hivi katika madhara ya kosa lake hilo la kimahesabu.

Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vile vile limesema, majibu makali ya jinai hiyo ya Marekani yatatolewa kwa wakati wake na katika eneo linalofaa kabisa. Taarifa ya baraza hilo imeongeza kuwa: Ni jambo lisilo na shaka kwamba jinai hiyo, ni kisasi kilicholipizwa na magaidi wa Daesh (ISIS) na Marekani dhidi ya nembo zilizojaa fakhari zilizosambaratisha ugaidi katika nchi za Iraq na Syria.

Kitendo cha kigaidi cha Marekani cha kumuua shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH na watu kadhaa muhimu aliokuwa amefuatana nao, usiku wa kuamkia jana Ijumaa, tarehe 3 Januari 2020 waliuliwa shahidi baada ya kushambuliwa kigaidi na helikopta ya Marekani karibu na uwanja wa ndege wa kimataifa wa Baghdad, mji mkuu wa Iraq. Shambulio hilo la kigaidi limezidi kudhihirisha kwamba Marekani ndicho kitovu cha vitando vya kigaidi na ndiye muhusika mkuu wa ukosefu wa amani na machafuko katika eneo hili. Kabla ya hapo pia, Marekani imeonesha mara chungu nzima kuwa ni adui wa harakati na mrengo wowote ule unaopambana na ugaidi.

Siku ya Jumatano ya wiki iliyopita, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alionana na maelfu ya wakunga kutoka kona zote za Iran na huku akigusia matamshi ya rais wa Marekani aliyetoa vitisho dhidi ya taifa la Iran kwa kudai kuwa eti Tehran ndiye muhusika mkuu wa matukio ya hivi karibuni ya nchini Iraq amesisitiza kuwa, Watu wote watambue kwamba Jamhuri ya Kiislamu haipendi vita, lakini mtu yeyote anayehatarisha manufaa, maslahi, heshima, utukufu na maendeleo ya taifa la Iran, bila ya shaka yoyote tutakabiliana naye vilivyo na kutoa pigo kubwa dhidi yake.

Ukweli wa mambo ni kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haijawahi hata mara moja kuanzisha vita, si kwenye eneo hili tu, bali hata nje yake, lakini muda wote imekuwa ikisimama imara kulinda usalama na heshima yake bila ya kumuogopa mtu yeyote. Mwezi Julai mwaka jana, wakati Marekani ilipofanya chokochoko za ujasusi ndani ya Iran kwa kutuma ndege yake ya kisasa kabisa ya RQ-4 Global Hawk katika masafa ya juu angani kusini mwa Iran kujaribu kujasisi, hata hivyo Iran haikuruhusu jambo hilo, iliitungua mara moja ndege hiyo ya adui.

Karibu na ndege hiyo isiyo na rubani ya Marekani, ilikuwepo ndege nyingine ya kijeshi ya Marekani iliyokuwa na wanajeshi 35 ambayo nayo iliingia bila ya ruhusa katika anga ya Iran. Jamhuri ya Kiislamuu ya Iran ilikuwa na uwezo wa kuitungua ndege hiyo pia kama ilivyoituhungua ile ya Global Hawk, lakini haikufanya hivyo.

Jarida la Time la kila wiki la Marekani lilimnukuu mwanachama mmoja mwandamizi wa Chuo cha "Taasisi ya Hoover" na "Taasisi ya Utafiti wa Kimataifa ya Freeman Spogli" ya Chuo Kikuu cha Stanford akisema kuwa: "Kutunguliwa droni hiyo ni aina fulani ya kuitumia ujumbe Marekani kwamba Iran tofauti na tunavyodhani, ina nguvu zaidi ya tunazofikiria."

Amma moja ya malengo makuu ya Marekani ni kutoa pigo kwa kambi ya muqawama katika eneo hili. Hata hivyo, chokochoko za Marekani za kuichokoza kambi ya muqawama zimewaweka kwenye hatari vibaraka na tawala za kidikteta za eneo hili zinazoshirikiana na dola hilo la kibeberu. Fikra za walio wengi duniani hivi sasa zinaihesabu Marekani na hasa rais wa nchi hiyo, Donald Trump kuwa ndio chanzo cha migogoro, vita na uvunjaji wa sheria za kimataifa.

Jinai ya usiku wa kuamkia jana Ijumaa ya kumuua kigaidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH imekuwa na taathira kimataifa na bila ya shaka yoyote waliotenda jinai hiyo watapata majibu makali katika kipindi kifupi tu kijacho na kwamba propaganda zao za muda mfupi hazitowasaidia kitu.

..........
340