Main Title

source : parstoday
Jumamosi

28 Novemba 2020

08:05:24
1089988

Iran italipiza kisasi mauaji ya mwanasayansi maarufu, shahidi Fakhrizadeh

Waziri wa Intelijensia wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa Iran italipiza kisasi kufuatia kuuawa shahidi Mohsen Fakhrizadeh ambaye alikuwa Mkuu wa Shirika la Utafiti na Ubunifu katika Wizara ya Ulinzi ya Iran.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Jana Ijumaa alasiri, Fakhrizadeh aliuawa shahidi baada ya gari lililokuwa limembeba kushambuliwa katika mji wa Absard katika eneo la Damavand mkoani Tehran.

Kwa mujibu wa taarifa, awali gari lililokuwa limesheheni bomu lilirupika na kisha ufyatulianaji risasi ukafuata baina ya walinzi wa Shahidi Fakhrizadeh na magaidi.

Waziri wa Intelijensia wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Mahmoud Alawi ametoa taarifa  ambapo amebainisha masikitiko yake kufuatia kuuawa kidhalimu mkuu wa Shirika la Utafiti na Ubunifu katika Wizara ya Ulinzi  ya Iran na kusisitiza kuwa vikosi vya usalama vya Iran vimeaza kuwasaka magaidi mamluki waliotekeleza jinai hiyo na kwamba italipiza kisasi damu ya shahidi huyu azizi kwa wahusika na wasababishaji wa jinai hii.

Idara ya Habari katika Wizara ya Ulinzi ya Iran imesema Shahidi Fakhrizadeh alijeruhiwa vibaya wakati wa mapigano baina ya walinzi wake na magaidi na kisha akakimbizwa hospitali na kufariki kufuatia majeraha yake. Shirika la Habari la Faris limesema watu watatu hadi wanne waliuawa katika mapigano hayo na wote walikuwa ni magaidi.

Wakati huo huo Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif amelaani vikali hujuma hiyo ya kigaidi na kuongeza kuwa, kuna dalili nzito zinazoonyesha kuwa utawala wa Kizayuni wa Israel ulihusika katika mauaji ya Fakhirzadeh, ambaye pia alikuwa profesa wa  fizikia katika Chuo Kikuu cha Imam Hussein mjini Tehran.

Katika ujumbe kupitia Twitter, Zarif ameandika: “Magaidi wamemuua mwanasayansi maarufu wa Iran leo. Kuna dalili nzito zinazoonyesha Israel imehusika na ni ishara ya wanavyotapatapa wapenda vita.”

Zarif ametoa wito kwa jamii ya kimataifa, hasa Umoja wa Ulaya kusitisha udumakuwili wenye kuaibisha na kulaani kitendo hiki cha kigaidi.

Naye mwenyekiti wa Kamandi Kuu ya Majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Meja Jenerali Mohammad Baqeri amesema hujuma hiyo ya kinyama imetekelezwa na magaidi wanaofungamana na uistikbari wa kimataifa na utawala wa kishetani wa Kizayuni. Amesema ingawa mauaji hayo ni pigo kwa sekta ya ulinzi ya Iran lakini maadui wafahamu kuwa, njia iliyofunguliwa ma wasomi kama Shahidi Fakhirzadeh haiwezi kufika ukingoni.”

Baqeri aidha amesema ulipizaji kisasi mkali unawasubiri waliotekeleza ugaidi huo kwani watafuatiliwa na kufikishwa kizimbani.

Kwa upande wake, Waziri wa Ulinzi wa Iran Brigedia Jenerali Amri Hatami amesema Shirika la Utafiti na Ubunifu katika Wizara ya Ulinzi  ya Iran, ambalo lilikuwa likisimamiwa na Shahidi Fakhirzadeh, lilikuwa mstari wa mbele kuunda vifaa vya kupima ugonjwa wa corona. Amesema pia alikuwa akiongoza jitihada za kuunda chanjo ya corona nchini na matokeo ya jitihada hizo yatatangazwa.

Huku akilaani mauaji hayo, Hatami amesema Fakhirzadeh alikuwa pia naibu waziri wa ulinzi, na mwanasayansi mashuhuri aliyekuwa na historia ndefu ya ubunifu na aliwapa mafunzo wanasayansi wengi kwa ajili ya ustawi wa kisayansi Iran.

Kwa mfano alihusika katika utumizi wa takenolojia ya miale ya laser katika kutambua ndege za adui pasina kutegemea radar.

Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Mahakama ya Iran Ibrahimi Raeisi amesema 'wasaliti wanaofungamana na ajinabi na Uzayuni wa kimataifa wametekeleza jinai kubwa kwa lengo chafu la kuzuia ustawi wa kisayansi nchini Iran. Huku akiwapongeza wanasayansi wa Iran kwa kuimarisha kasi ya ustawi wa Iran katika sekta mbali mbali za sayansi, ikiwemo sekta ya nyuklia, Raeisi amesema kuuawa shahidi Fakhirzadeh hakutasitisha mkondo wa ustawi wa Iran.


342/