Main Title

source : Parstoday
Jumamosi

9 Januari 2021

14:56:36
1104438

Mtazamo wa Kiongozi Muadhamu; fedheha ya kidemokrasia ya Marekani na mustakabali wa JCPOA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa hotuba muhimu kwa mnasaba wa siku ya leo ya maadhimisho ya mapambano ya Dei 19 ya wananchi wa Qum dhidi ya utawala wa kiimla wa Shah ambapo ameashiria matukio ya hivi karibuni nchini Marekani, sharti la Iran la kurejea Washington katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na uwepo wa kieneo na uwezo wa kiulinzi wa Iran.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Ayatullahi Sayyid Ali Khamenei amesema katika hotuba yake hiyo kwa njia ya televisheni kwamba, mapambano ya wananchi wa Qum ilikuwa harakati dhidi ya Marekani na kusisitiza kuwa, harakati ya tarehe 19 inahesabiwa kuwa ilikuwa pigo la nyundo la Kiibrahim dhidi ya sanamu kubwa, mapigo ambayo yangali yanaendelea hadi leo hii.

Katika hotuba yake hiyo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria siasa za Marekani dhidi ya Iran katika duru mbalimbali za historia ambapo katika tathmini yake kuhusiana na matukio ya hivi karibuni nchini Marekani, amesema kuwa, hali ya leo ya kisiasa na kiuchumi ya nchi hiyo ni ya fedheha.

Hali ya uchaguzi wa Marekani imeumbua na kufedhehesha utendaji mbovu wa demokrasia ya kiliberali ya nchi hiyo na kwamba, uvamizi na hujuma iliyofanywa na wananchi wa Marekani dhidi ya jengo la Kongresi ya nchi hiyo imekuwa sababu ya kufanyiwa mzaha na dharau Marekani na maadui bali hata marafiki zake ulimwenguni. Hii leo demokrasia, haki za binadamu na thamani za Marekani sio kigezo tena kwa wengine, kwani uchaguzi wa Novemba mwaka jana wa nchi hiyo umethibitisha utendaji mbovu wa yote hayo.

Katika kutoa tahmini yake kuhusiana na hali ya masiku haya ya Marekani na uvamizi dhidi ya jengo la Kongresi nchini humo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameaashiria tukio la fitina ya 1388 (2009) iliyoibuka hapa nchini baada ya uchaguzi wa Rais na kusema kuwa, kile ambacho Wamarekani walikuwa wakitaka kulitwisha taifa hili kupitia tukio la fitina ya 2009 kimewakumbuka wenyewe katika mwaka huu wa 2021.

Hali ya leo ya Marekani imeonyesha kilele cha ukosefu wa uthabiti ambapo hata viongozi wa nchi hiyo wamesema kuwa, matukio ya juzi tarehe 6 Januari ni doa baya katika historia ya Marekani, na kwa maneno mengine ni kuwa, huu ni mwanzo wa enzi za baada ya Marekani.

Katika fremu hiyo, Barack Obama Rais mstaafu wa Marekani amesema katika radiamali yake kwa fujo na vurugu zilizoibuka katika jengo la Kongresi ya nchi hiyo kuwa, hili doa jeusi katika historia ya Marekani. Richard Haass, Mkuu wa Chuo cha Mahusiano ya Kigeni cha Marekani naye amesema katika tathmini yake kuhusu machafuko na fujo katika jingo la Kongresi kwamba: Ni jambo lililo mbali kutokea mtu ulimwengu akaiheshimu tena Marekani; na kama enzi za baada ya Marekani zitakuwa zimeanza, basi hapana shaka kuwa, hilo lilianza Januari 6.

Vikwazo, uwepo wa Iran katika eneo, nguvu zake za kiulinzi na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA ni mambo mengine yaliyoashiriwa na Kiongozi Muadhamu wa Mpainduzi ya Kiislamu ambapo amebainisha nukta muhimu pia katika masuala hayo. Viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu wamesisitiza mara chungu nzima kwamba, ulimwengu wa Magharibi na maadui wa taifa la Iran wanapaswa kuhitimisha vikwazo vyao vya kidhulma dhidi ya taifa hili. Vikwazo dhidi ya Iran ilikuwa jinai ambayo iliendelea kufanywa hata katika kilele cha maradhi ya Corona.

Hii leo baadhi ya madola ya Ulaya sambamba na kubadilika uongozi nchini Marekani, yakiwa na lengo la kuhifadhiwa na kubakishwa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA yamekuwa yakizungumzia suala la uwepo wa Iran katika eneo la uwezo wake wa kiulinzi huku yakipuuza na kufumbia macho asili ya mazungumzo ambayo ni kuondolewa vikwazo vyote ilivyowekewa taifa hili. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi wa Kiislamu amezungumzia suala hilo kwa kusema: Maana na mantiki ya Iran kuwepo katika eneo ni kuwapa nguvu marafiki na waungaji mkono wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuongeza kuwa: "Uwepo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika eneo unaleta uthabiti na unapelekea kuondoa ukosefu wa uthabiti kama ilivyoshuhudiwa huko Syria na Iraq na huu ni ukweli ambao wote wanaufahamu; kwa msingio huo uwepo huu ni wa hakika na unapaswa kuwepo na utaendelea kuwepo."

Kuhusiana na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA baada ya upande wa pili kuzembea na kutotekeleza ahadi zake, serikali ya Iran katika hatua yake ya karibuni ya nyuklia, imetekeleza kivitendo katiba na kuanza urutubishaji wa madini ya urani wa asilimia 20.

Iran kama yalivyo mataifa mengine ina haki kwa mujibu wa JCPOA ya kutekeleza ahadi zake na kwa maneno mengine ni kuwa, ‘utekelezaji ahadi mkabala na utekelezaji ahadi’ ni jambo ambalo limebainishwa wazi katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA. Katika mazingira kama haya, endapo Iran itanufaika kikamilifu kiuchumi kwa mujibu ya JCPOA, yaani vikwazo vyote dhidi yake vikaondolewa kikamilifu, basi wakati huo kurejea Marekani katika JCPOA kutakuwa na maana na Iran nayo itarejea katika mchakato wa kutekeleza ahadi zake.

342/