Main Title

source : Parstoday
Jumapili

14 Julai 2024

15:44:17
1472045

Tukio la kupigwa risasi Trump; ishara ya kuongezeka ghasia za kisiasa nchini Marekani

Tukio la kupigwa risasi Donald Trump, rais wa zamani wa Marekani wakati akizungumza kwenye kampeni ya uchaguzi mbele ya wafuasi wake huko Butler, Pennsylvania, Jumamosi jioni, huku uchaguzi wa rais ukikaribia kufanyika nchini humo, limeibua gumzo kubwa la kisiasa katika vyombo vya habari vya Marekani.

Jana Jumamosi, mtu mmoja alifyatua risasi na kumpiga sikio la kulia Trump, alipokuwa akihutubia wafuasi wake huko Pennsylvania. Richard Goldinger, mwendesha mashtaka wa mji wa Butler, ametangaza kuwa watu wawili wameuawa na mwingine wa tatu kujeruhiwa vibaya katika tukio hilo la ufyatuaji risasi lililomlenga Trump. Polisi wa FBI wanaenelea na uchunguzi kuhusui tukio hilo na tayari Trump ameruhusiwa kutoka hospitalini.

FBI imetangaza jina la mtu aliyejaribu kumuua Donald Trump kuwa ni Thomas Matthew Crooks mwenye umri wa miaka 20. Kabla ya kumpiga risasi Trump, Crooks alisambaza video akisema: 'Mimi ni Thomas Matthew Crooks, ninawachukia Warepublican, namchukia Trump.'

Tukio la kumpiga risasi Trump linaweza kuonekana kama ishara nyingine ya kuongezeka ghasia za kisiasa nchini Marekani, ghasia  ambazo zimeongezeka katika miaka ya hivi karibuni, hasa baada ya kuvamiwa Congress ya Marekani na wafuasi wa Trump mnamo Januari 6, 2021. Kwa hakika, Trump mwenyewe amefikwa na jambo ambalo yeye mwenyewe amekuwa akilichochea wakati wa kampeni zake za uchaguzi.

Akizungumzia tukio la kupigwa risasi Trump, Rais Joe Biden wa Marekani ambaye ni mgombea mpinzani wa Trump amedai kuwa ghasia hazina nafasi katika jamii ya Marekani. Viongozi wengi wa zamani na wa sasa wa Marekani pia wameleaani jaribio hilo la kigaidi dhidi ya Trump. Barack Obama, rais wa zamani wa Marekani ameandika kwenye mtandao wa X kwamba: "Vurugu za kisiasa kazina nafasi kabisa katika demokrasia yetu." Trump Junior, mtoto wa kwanza wa Trump, pia ametoa taarifa akisema: "Mbali na yale ambayo mrengo wa kushoto unamtuhumu (Trump) kuhusika nayo, ni wazi kuwa hataacha mapambano kwa ajili ya kuikomboa Marekani." Amelitaja tukio hilo katika mtandao wa X kuwa ni tukio la kigaidi.

Uchunguzi wa historia ya Marekani unaonyesha wazi kwamba viongozi wa kisiasa na wanaharakati wa kisiasa na kijamii wa nchi hiyo daima wamekuwa walengwa wa vurugu za kisiasa na ugaidi. Mfano wa wazi wa suala hili ni mauaji ya kigaidi shisi ya aliyekuwa Rais wa Marekani John F. Kennedy huko Dallas, Texas Novemba 1963, mauaji ya mgombea wa chama cha Democratic, Robert Kennedy Juni 1968 huko Los Angeles, California, na mauaji ya Martin Luther King, kiongozi wa vuguvugu la haki za kiraia la Wamarekani mwenye asili ya Afrika huko Memphis, Tennessee mnamo Aprili 1968. Hivyo, katika nchi ambayo rais, mgombea wa urais na viongozi wengine wa mapambano ya kiraia wameuawa kigaidi, jaribio la kutaka kumuua Donald Trump sio tukio la kushangaza.

Kwa upande mwingine, jamii ya Marekani, hasa baada ya tukio la mashambulizi dhidi ya Bunge la Congress mnamo Januari 2021, imekumbwa na hali inayoongezeka kila siku ya mivutano na vurugu za kisiasa, ambapo moto wa tofauti za kisiasa na kiitikadi unazidi kuwaka. Katika kampeni zao za uchaguzi, Joe Biden na Donald Trump wamekuwa wakirushiana maneno makali, kila mmoja akimtuhumu mwenzake kuwa anataka kuiangamiza Marekani. Hivyo katika hali kama hiyo si jambo la kushangaza kumuona mtu mwenye misimamo mikali ya mrengo wa kulia akichukua hatua ya kutaka kumuua kigaidi mmoja wa wagombea wa uchaguzi ujao wa rais, tena katika jamii ambayo upatikanaji wa silaha ni rahisi kuliko upatikanaji wa vitabu, na silaha ni nyingi kuliko idadi ya wakazi wake. Ikiwa vita na mapigano juu ya uchaguzi yalifikia kilele katika shambulio la Bunge la Merikani mnamo 2020 baada ya kufanyika uchaguzi, sasa mwaka huu 2024, vita na mapigano yanafanyika kabla ya uchaguzi.

Suala jingine linalopaswa kuashiriwa hapa ni hatua ya Trump ya kutaka kutumia fursa hiyo kwa maslahi yake binafsi ya kisiasa kwenye uchaguzi. Amejaribu kulifanya tukio hilo lionekane kuwa kubwa kupita kiasi na kuonyesha kuwa amedhulumiwa ili kujaribu kuvutia uungaji mkono wa wapiga kura, na hasa wale ambao hadi sasa hawajaamua watampigia nani kura. Kwa maneno mengine, mshindi wa jaribio hilo la kigaidi dhidi ya Trump ni Trump mwenyewe. Wakati huo huo mivutano na ugomvi wa uchaguzi unaonekana wazi katika kambi ya Rais Joe Biden katika chama cha Democratic ambapo kuna uwezekano mkubwa wa rais huyo kupigwa kumbo chamani na mgombea mwingine kuarifishwa kuchukua nafasi yake ili apate kuchuana na Trump katika uchaguzi ujao.

Kwa ujumla, kuna uwezekano mkubwa kwamba baada ya tukio la kumpiga risasi Trump, idadi ya wafuasi wake itaongezeka katika majimbo mbalimbali ya Marekani na hivyo kuongeza nafasi yake ya kushinda uchaguzi wa rais wa Novemba 2024.

342/