Mamia ya waumini wa Wilaya ya Kondoa, Dodoma, walikusanyika tarehe 04/02/2026 kuadhimisha Mazazi Matukufu ya Imam Mahdi (a.t.f.s). Khatibu wa Majlisi, Sheikh Abdul-Latif, aliwakumbusha Waislamu umuhimu wa kuwatambua na kuwatetea viongozi wao, akionya kuwa maadui hutumia njama kuvuruga mihimili ya jamii ili kuiharibu ustaarabu wake.
Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Sherehe za Maadhimisho ya Mazazi ya Imam Mahdi (a.s) zilifanyika kwa mafanikio makubwa tarehe 04 Februari 2026 katika Wilaya ya Kondoa, Mkoa wa Dodoma, zikihudhuriwa na waumini kutoka maeneo mbalimbali.
Khatibu wa Majlisi hiyo tukufu alikuwa Sheikh Abdul-Latif, ambaye katika khutba yake aliusisitiza Umma kuwa ni wajibu wao kuwasoma, kuwajua na kuwaheshimu viongozi wao wa kidini na kijamii, kwani wao ndio washika hatamu wa maendeleo ya jamii yoyote.
Sheikh Abdul-Latif alieleza kuwa mataifa ya Magharibi hutumia kila mbinu kujenga ukuta baina ya jamii na viongozi wake kwa kutengeneza skendo, tuhuma na chuki, ili jamii iwakimbie viongozi wao na hivyo iwe rahisi kutawaliwa na malengo ya kigeni.
Katika hotuba yake alisema:
“Ukitaka kuibomoa jamii na kuharibu ustaarabu wowote, hakikisha unavunja mihimili mikuu mitatu.”
Kisha akaitaja mihimili hiyo kuwa ni:
Kwanza – Uongozi:
Kutengeneza skendo, tuhuma na shaka dhidi ya viongozi hadi wananchi wawachukie na waache kuwafuata.
Pili – Mama:
Kuondoa heshima ya mwanamke kuitwa mama wa nyumbani, kumfanya aone aibu kulea familia, na kumsukuma kuacha jukumu la malezi ili kuporomoka maadili ya jamii.
Tatu – Walimu na Masheikh:
Kujenga dharau kwa walimu, Masheikh na watu wa elimu ili jamii isiwaone kuwa ni muhimu tena.
Sheikh Abdul-Latif alihitimisha kwa kusema kuwa endapo mihimili hiyo mitatu itabomolewa, basi jamii itakuwa imeharibiwa na ustaarabu wake kuvunjwa.
Maadhimisho hayo yaliambatana na dua, qasida na mawaidha yaliyoamsha ari ya mapenzi kwa Imam wa Zama (a.t.f.s) pamoja na wajibu wa Umma katika kujenga jamii bora yenye maadili na utii kwa viongozi wa haki.
Your Comment