Wakiongozwa na azma ya kumfuata Mtume (saww) kama kielelezo bora cha maisha ya Kiislamu, wanafunzi wa Hawzat Hazrat Zainab (sa) Kigamboni wameanzisha ratiba maalum ya kila siku ya usomaji wa Qur’an Tukufu katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhan, kwa lengo la kuimarisha malezi yao ya kiimani na kunufaika kikamilifu na baraka za Mwezi huo Mtukufu, ikiwemo faida za kimwili, kiroho na kijamii.
Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Katika kuuenzi Mwezi Mtukufu wa Ramadhan kama mwezi wa Qur’an Tukufu, wanafunzi wa Hawzat Hazrat Zainab (sa) kilichopo Kigamboni, Dar es Salaam, wameendelea kudumisha ratiba maalum ya kila siku ya usomaji wa Qur’an Tukufu ikiwa ni sehemu ya ibada na malezi yao ya kiroho.
Ratiba hiyo inatekelezwa kwa nidhamu na kujituma, ambapo mabinti wa Kiislamu wa chuo hicho hukusanyika kwa pamoja kusoma, kutafakari na kujadili aya za Qur’an Tukufu, wakilenga kuimarisha uhusiano wao na Mwenyezi Mungu (swt) katika mwezi huu adhimu.
Uongozi wa chuo umeeleza kuwa Ramadhan ni fursa adhimu ya kujijenga kiroho na kimaadili, huku Qur’an Tukufu ikiwa ndio mwongozo mkuu wa maisha ya Muislamu. Hivyo, kuipa nafasi ya pekee katika ratiba za kila siku ni sehemu ya kutekeleza kwa vitendo mafunzo ya Uislamu.
Malezi yanayotolewa katika chuo hicho yanajengwa juu ya msingi wa kufuata mafunzo ya Mtume Muhammad (saww), kama inavyobainishwa katika Qur’an Tukufu: “Na hakika mmekuwa na kielelezo chema kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu…”
Aya hii inawahimiza Waumini kumfanya Mtume kuwa ruwaza katika ibada, maadili na mwenendo wa maisha. Kwa kutambua hilo, wanafunzi wa Hawzat Hazrat Zainab (sa) wanajitahidi kuhuisha Sunnah ya Mtume (saww) kwa kuipa Qur’an nafasi kuu katika safari yao ya kiroho.
Aidha, Ramadhan umetajwa kuwa ni kama “chuo kikuu cha subira na uvumilivu,” mwezi ambao Waislamu kote duniani huutumia kama darasa la kujifunza kujidhibiti, kuongeza ibada, kufanya amali njema na kujiepusha na makatazo ya Mwenyezi Mungu (swt).
Kupitia ratiba hiyo ya kila siku ya usomaji wa Qur’an, chuo kinaendeleza lengo lake la kuwalea wanafunzi katika misingi ya taqwa, elimu na maadili mema, ili waweze kuwa wanawake wa Kiislamu wenye mchango chanya katika jamii.
Programu hiyo imeendelea kupokelewa kwa hamasa kubwa miongoni mwa wanafunzi, ikidhihirisha kiu ya kizazi cha sasa katika kurejea kwa dhati kwenye Qur’an Tukufu kama mwongozo wa maisha.
Your Comment