Majlisi ya tano ya maombolezo ya Imam Hussein (a.s.) ilifanyika katika Msikiti wa Ahlul-Bayt (a.s) mjini Moshi, ambapo Khatibu Sheikh Dkt. Abdul Razaq Amir alizungumzia mada isemayo: “Vijana wanajifunza nini kutokana na Karbala?”

25 Juni 2026 - 18:07

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (a.s.) –ABNA–, Majlisi ya tano ya maombolezo ya Imam Hussein (a.s.) ilifanyika katika Msikiti wa Ahlul-Bayt (a.s) Mjini Moshi, Tanzania, ikihudhuriwa na Waumini Wapenzi wa Ahlul-Bayt (a.s) kutoka maeneo mbalimbali ya mji huo.
 
Katika majlisi hiyo, Khatibu, Sheikh Dkt. Abdul Razaq Amir, aliwasilisha mada yenye anuani isemayo: “Vijana wanajifunza nini kutokana na Karbala?”, akibainisha kuwa tukio la Karbala ni shule ya milele inayowafundisha vijana maadili, ujasiri na kusimama upande wa haki.
 
Alieleza kuwa Imam Hussein (a.s) na vijana waliokuwa pamoja naye katika Karbala walitoa mfano wa kujitolea, subira na utiifu kwa Mwenyezi Mungu, huku wakionesha umuhimu wa kutetea ukweli hata katika mazingira magumu.
 
Sheikh Dkt. Abdul Razaq Amir aliwahimiza vijana kuiga tabia za mashujaa wa Karbala kwa kujenga uchamungu, kuzingatia maadili mema, kuwapenda Ahlul-Bayt (a.s) na kuwa tayari kuutetea ukweli na haki katika jamii.
 
Aidha, alisisitiza kuwa Karbala inawafundisha vijana kuwa na msimamo thabiti mbele ya dhulma, kutokubali kupotoshwa na kuishi maisha yenye malengo ya kumridhisha Mwenyezi Mungu.
 
Washiriki wa majlisi hiyo walielezwa pia kuwa kumbukumbu za Imam Hussein (a.s) zinaendelea kuwa chanzo cha mwamko wa kiroho na mafunzo muhimu kwa kizazi cha vijana, na kwamba ujumbe wa Karbala unabaki kuwa nuru inayowaongoza Waumini katika nyakati zote.

Your Comment

You are replying to: .
captcha