Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) - ABNA - Jana, Alhamisi, tarehe 5 Mei, 2025, Sheikh Ridhwa M. Dosa, Mkurugenzi wa Kituo cha Soma Qur’an, kilicho chini ya Taasisi ya Khatamul Anbiyaa inayoongozwa na Al-Haji Ghulamu-Hussen Mukhtar, alipokea kwa heshima kubwa mgeni maalum kutoka mji Mtakatifu wa Qom, Iran, Sayyid Dhamir Abasi Jafariy, mwenye asili ya India.
Ukaribisho wa Kiroho
Hafla ya mapokezi ilianza kwa ufunguzi wa kisomo cha Qur’an Tukufu kilichosomwa kwa umahiri na heshima kubwa na Qari Alawiy Yasini, mwanafunzi wa kituo cha Soma Qur’an, kinachojihusisha na kukuza elimu ya usomaji wa Qur’an kwa vijana na watu wazima katika Mkoa wa Arusha.
Nasaha za Sayyid Dhamir Abasi Jafariy
Baada ya kisomo hicho, mgeni alitoa nasaha zenye mguso mkubwa kuhusu nafasi ya Qur’an Tukufu katika maisha ya Mwislamu na umuhimu wa kuambatana na Ahlul-Bayt (a.s) kama waongozaji wa haki baada ya Mtume Muhammad (saww). Alisisitiza kuwa mafanikio ya kweli ya kiroho na kijamii hayawezi kupatikana bila mafundisho ya pamoja ya Qur’an na kizazi cha Mtume (a.s).
Hitimisho la Hafla
Tukio hilo lilihitimishwa kwa dua iliyojaa unyenyekevu kwa Mwenyezi Mungu, iliyoongozwa na Haji Ghulamuhusen Mukhtar, Mkurugenzi wa Taasisi ya Khatamul Anbiyaa – taasisi inayojishughulisha na elimu, maadili na huduma za kijamii kwa jamii ya Kiislamu nchini Tanzania.
Maoni ya Washiriki
Walioshiriki walieleza kuguswa na ujumbe wa kiroho wa mgeni huyo na kupongeza juhudi za Kituo cha Soma Qur’an katika kukuza kizazi cha wahifadhi na wasomaji wa Qur’an.
Habari hii ni kwa hisani kubwa:
Idara ya Habari – Taasisi ya Khatamul Anbiyaa
Arusha, Tanzania.
Your Comment