JMAT imesisitiza kuwa kusaidia kazi za mikono kwa wananchi ni njia madhubuti ya kuondoa umaskini na kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja. Jumuiya hiyo imetoa wito kwa Watanzania kuendeleza mshikamano wa kitaifa na kumuomba Mungu aendelee kuilinda nchi kwa amani na utulivu ili kazi za maendeleo ziendelee kufanyika kwa mafanikio.
Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT), chini ya uongozi wa Mwenyekiti wake, Dr. Alhad Mussa Salum, imefanya ziara maalum katika soko la kisasa la nyama choma la Kumbilamoto lililopo Vingunguti, Jiji la Dar es Salaam-Tanzania, kwa lengo la kujionea maendeleo ya mradi huo wa kimkakati na kutambua mafanikio ya Serikali katika kuboresha maisha ya Wananchi.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Dr. Alhad alisema:
"Tunashukuru kwa kualikwa kutembelea mradi huu wa kimkakati na wa kombozi kwa wananchi. Maendeleo tuliyoyaona hapa yametufurahisha sana. Tumeridhika kuona kuwa wananchi wameondokana na adha walizokuwa wakizipata wakati wa jua kali na mvua. Tunatoa pongezi kwa Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuweka mazingira bora ya kazi kwa watu wa kipato cha chini."
JMAT imesisitiza kuwa kusaidia kazi za mikono kwa wananchi ni njia madhubuti ya kuondoa umaskini na kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja. Jumuiya hiyo imetoa wito kwa Watanzania kuendeleza mshikamano wa kitaifa na kumuomba Mungu aendelee kuilinda nchi kwa amani na utulivu ili kazi za maendeleo ziendelee kufanyika kwa mafanikio.
Katika ziara hiyo, Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Mhe. Omary Kumbilamoto, alieleza kuwa serikali inaendelea kuwekeza kwenye miundombinu ya masoko ili kuwainua wananchi kiuchumi. Alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa uwekezaji huo pamoja na Mkurugenzi wa Jiji, Ndugu Elihuruma Mabelya, kwa usimamizi bora uliohakikisha mradi unakamilika kwa viwango vya kisasa.
Soko hilo la kisasa linatarajiwa kuhudumia zaidi ya wafanyabiashara 232, wakiwemo wauzaji wa nyama choma, mama lishe, wauzaji wa vinywaji, mboga mboga na viungo mbalimbali. Pia, soko hilo linatarajiwa kuongeza mapato ya Halmashauri ya Jiji kwa wastani wa shilingi milioni 11 kila mwezi, ambayo ni zaidi ya shilingi milioni 100 kwa mwaka. Mradi huo umegharimu shilingi milioni 700 hadi kukamilika kwake.
Your Comment