Majlisi hii muhimu ilihudhuriwa na Waumini takriban 300 kutoka maeneo mbalimbali, waliokusanyika kwa pamoja kwa ajili ya kuadhimisha na kutafakari juu ya msimamo wa Imam Hussein (as) na ujumbe wake wa haki, uadilifu, na kujitolea kwa ajili ya kuihami na kuidumisha Dini Tukufu ya Mwenyezi Mungu (s.w.t).
Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Kwa Taufiki na Rehema za Mwenyezi Mungu (s.w.t), leo hii (jana) tarehe: 3 Muharam 1447H (29 – 06 – 2025) Taasisi ya Kiislamu ya “Hujjatul Asr Society Of Tanzania” chini ya Uongozi na Usimamizi wa Maulana Sayyid Arif Naqawi (Hafidhahullah), imesimamia kwa mafanikio Majlisi ya Imam Hussein (as) iliyofanyika katika Masjid Imam Hassan (as), iliyopo maeneo ya Mandela, Ikwiriri - Tanzania.
Majlisi hii muhimu ilihudhuriwa na Waumini takriban 300 kutoka maeneo mbalimbali, waliokusanyika kwa pamoja kwa ajili ya kuadhimisha na kutafakari juu ya msimamo wa Imam Hussein (as) na ujumbe wake wa haki, uadilifu, na kujitolea kwa ajili ya kuihami na kuidumisha Dini Tukufu ya Mwenyezi Mungu (s.w.t).
Katika hotuba yake ya wazi na yenye kugusa nyoyo, Maulana Sayyid Arif Naqvi aliwasilisha ujumbe mzito wa Imam Hussein (as) kwa hadhira ya Waumini, akiwasihi kuwa na hima na shauku ya kumjua zaidi Imam Hussein (as) kupitia usomaji, tafakuri, na kuhudhuria Majlisi kama hizi za Muharam, ili waweze kufaidika zaidi kimaarifa, kiroho na kimaadili.
Tukio hili la Maombolezo katika Mwezi wa Muharram limekuwa ni sehemu ya juhudi za Tabligh (kueneza ujumbe wa ukweli na haki) ambazo zinaendelea kufanywa na Taasisi ya Kiislamu ya “Hujjatul Asr Society of Tanzania”, chini ya mwamvuli wa Imani, Mshikamano, na Kujitolea kwa ajili ya kuendeleza Mafundisho ya Ahlul-Bayt (a.s).
Tunashukuru Waumini wote walioshiriki na wanaoendelea kushiriki katika Majalisi hizi za Maombolezo ya Shahada ya Imam Hussein (as), na tunaendelea kuhamasisha jamii zaidi kujumuika katika Majlisi zinazofuata ili kuimarisha uelewa wa Dini na kuenzi Historia halisi ya Karbala.
Ripoti hii inakujieni kwa hisani kubwa ya: Mtumishi wa Hujjatul Asr Society Of Tanzania
Your Comment