Kwa mujibu wa waandaaji, mikusanyiko kama hii itaendelea katika siku zijazo za Mwezi Mtukufu wa Muharram mpaka Arubaini ya Imam Hussein (as), kwa ajili ya kuendelea kujifunza zaidi na kuhimiza amani, mshikamano wa Waislamu, na kuenzi misingi ya Kiislamu kama ilivyofundishwa na Ahlul Bayt (a.s).
Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Mombasa, 23 Julai 2025 – Majlisi maalumu za kuomboleza tukio la Karbala zimeendelea kwa mafanikio makubwa Jijini Mombasa, huku mamia ya waumini wafuasi wa Ahlul-Bayt (as) wakikusanyika katika Ukumbi wa Bilal kusikiliza mawaidha yaliyojaa hekima, mafunzo na mwanga wa kihistoria.
Majlisi hizi ziliendeshwa na Sayyida Zena Saggaf, mzungumzaji maarufu na mfasiri wa harakati za Ahlul Bayt (a.s) na mafunzo yake, ambaye kwa ufasaha mkubwa aliangazia maana ya Karbala katika maisha ya leo, umuhimu wa kusimama na haki, na wito wa kujitathmini katika kipindi hiki cha Muharram.
Katika hotuba yake, Sayyida Zena aligusia jinsi tukio la Karbala linavyoendelea kuwa kioo cha kupambanua baina ya dhulma na uadilifu, akisisitiza kwamba ujumbe wa Imam Hussein (a.s) bado una nguvu na uhalisia katika jamii ya leo inayokabiliwa na changamoto mbalimbali za kijamii, kiroho na kiadili.
Waumini walionekana kuguswa kwa kiasi kikubwa na mawaidha hayo, wakitokwa na machozi na kubaki kimya katika tafakuri nzito kuhusu madhila ya familia ya Mtume (s.a.w.w) na wajibu wa waumini katika kuendeleza njia ya haki.
Majlisi hizi zimeendelea kuwa jukwaa muhimu la kuelimisha, kuimarisha mshikamano wa waumini, na kuamsha dhamira ya kutetea uadilifu katika jamii.

Your Comment