“Elimu ya Dini ya Kiislamu ndiyo msingi na kipaumbele cha kwanza ndani ya BAKWATA. Kila kiongozi anatakiwa kujitokeza na kushiriki kikamilifu katika shughuli yoyote inayohusu maendeleo ya chuo cha Daarul Maarif.”
Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Dar es Salaam, Alhamisi 31 Julai 2025, Sheikh Mkuu wa Tanzania, Mheshimiwa Mufti Dr. Abubakar Zubeir, jana Jumatano ameongoza kikao kizito cha maandalizi ya hafla maalumu ya mahafali ya Chuo cha Daarul Maarif Islamic Seminary, tukio ambalo linatarajiwa kufanyika kuanzia Ijumaa tarehe 1 hadi Jumapili tarehe 3 Agosti 2025, katika Makao Makuu ya BAKWATA, Kinondoni, Dar es Salaam.
Katika kikao hicho, Mufti aliwakumbusha viongozi wote wa ngazi za juu wa BAKWATA kutoka Makao Makuu na Mikoa mbalimbali kuwa:
“Elimu ya Dini ya Kiislamu ndiyo msingi na kipaumbele cha kwanza ndani ya BAKWATA. Kila kiongozi anatakiwa kujitokeza na kushiriki kikamilifu katika shughuli yoyote inayohusu maendeleo ya Chuo cha Daarul Maarif.”
Mufti aliagiza kuwa viongozi wote wa BAKWATA, kutoka Makao Makuu hadi Mikoani, wahakikishe wanahudhuria hafla hiyo muhimu bila kukosa, kwa lengo la kuonesha mshikamano na kuipa elimu ya Dini heshima yake inayostahili.
Kikao hicho pia kilihudhuriwa na viongozi wakuu akiwemo:
Katibu Mkuu wa BAKWATA, Alhaj Nuhu Mruma (ambaye pia ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi),
Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu, Alhaj Mataka, Naibu Katibu Mkuu (Dini), Alhaj Mohammed Khamis, Naibu Katibu Mkuu (Utawala na Fedha), Alhaj Mwenda, Katibu wa Mufti, Sheikh Mussa Hemed, Wakurugenzi wa Idara mbalimbali, Viongozi wa JUWAKITA (Jumuiya ya Wanawake wa Kiislamu Tanzania) na JUVIKIBA (Jumuiya ya Vijana wa Kiislamu BAKWATA), pamoja na maafisa wengine waandamizi.
Habari hii ni kwa hisani kubwa ya:
Dr. Harith Nkussa
Msemaji Maalum wa Mufti.
Your Comment