Madarasa kama haya ya Qur’an Tukufu yanayofanywa kila Siku ya Alhamisi kupitia Chuo cha Jamiat Al-Mustafa (s), Dar-es-salaam - Tanzania ni sehemu ya juhudi endelevu za kuimarisha Elimu ya Dini Tukufu ya Kiislamu na kueneza Mafundisho safi ya Ahlul-Bayt (as) Mashariki ya Kati na Barani Afrika kwa ujumla.
Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Alhamisi, 31 Julai 2025 – Kama ilivyo desturi ya kila siku ya Alhamisi, Darasa la Qur’an Tukufu limeendelea kufanyika katika Chuo cha Jamiat Al-Mustafa (as) kilichopo Dar es Salaam, Tanzania, chini ya uongozi na ufundishaji wa Alhaj Sheikh Muhammad Jafari.
Katika darasa la leo, msisitizo uliwekwa juu ya nafasi ya Qur’an katika kuhuisha jamii na kuleta umoja wa Waislamu, kwa kurejea katika mafundisho ya Qur’an na Ahlul-Bayt (as).
Katika kulihusianisha jambo hili, Sheikh Jafari alitaja maneno ya hekima ya Imam Ali (a.s) katika sehemu ya pili ya Hotuba ya 127 kutoka Nahjul Balagha, akisema:
«فَإِنَّمَا حُكِّمَ الْحَكَمَانِ لِيُحْيِيَا مَا أَحْيَا الْقُرْآنُ وَ يُمِيتَا مَا أَمَاتَ الْقُرْآنُ، وَ إِحْيَاؤُهُ الِاجْتِمَاعُ عَلَيْهِ وَ إِمَاتَتُهُ الِافْتِرَاقُ عَنْهُ، فَإِنْ جَرَّنَا الْقُرْآنُ إِلَيْهِمُ اتَّبَعْنَاهُمْ وَ إِنْ جَرَّهُمْ إِلَيْنَا اتَّبَعُونَا."
“Waamuzi wawili walihukumu wawe hai maadam ni wenye kuhuisha Qur’an, na waangamie (wauawe) madam wameua Qur’an. Kuhuisha Qur’an ni kukusanyika juu ya (Hukumu zake) Maamrisho yake, na kuiua Qur’an ni kutengana na hukumu zake. Basi ikiwa Qur’an itatuvuta kwao, tutawafuata; na ikiwa Qur’an itawavuta wao kwetu, basi ni wajibu wao kutufuata.”
Ufafanuzi Kuhusiana na Maneno Hayo:
Maneno haya yanasisitiza kuwa Qur’an ndiyo kipimo cha haki na uongozi, na kwamba mshikamano wa Waislamu unatokana na kushikamana nayo, huku mgawanyiko ukitokea pale inapopuuzwa.
Kwa ibara nyingine:
Maneno hayo ni Maneno ya Hekima kutoka kwa Imam Ali (a.s) yanayopatikana ndani ya Nahjul Balagha, Hotuba ya 127.
Maneno hayo, yanaashiria wazi kuwa kutozingatia mafundisho ya Qur’an ni sababu ya kupotea na kuangamia kwa Mwanadamu. Ni kwa kushikamana nayo ndipo jamii huweza kuhuishwa, kuunganishwa, na kuongozwa katika nuru ya Haki.
Kwa hiyo, ni wajibu wa kila mmoja wetu kutumia njia mbalimbali - Darsa Mahsusi za Kielimu za Qur'an, Mawasiliano katika masuala ya Quran, kutumia vyombo vya habari na mihadhara katika kueneza Mafundisho ya Qur'an n.k - ili kufikisha na kufasiri kwa kina maana ya Aya Tukufu za Qur’an Tukufu na Mafundisho ya Mwenyezi Mungu yanayoiongoza na kuijenga Jamii ili iwe ni Jamii iliyokuwa bora.
Kwa Mantiki hiyo, Madarasa kama haya ya Qur’an Tukufu yanayofanywa kila Siku ya Alhamisi kupitia Chuo cha Jamiat Al-Mustafa (s), Dar-es-salaam - Tanzania ni sehemu ya juhudi endelevu za kuimarisha Elimu ya Dini Tukufu ya Kiislamu na kueneza Mafundisho safi ya Ahlul-Bayt (as) Mashariki ya Kati na Barani Afrika kwa ujumla.
Your Comment