Tukio la Ghadir Khum na Tangazo la Wilayat: Tarehe na sehemu ya tukio (18 Dhulhijjah, Ghadir). Kauli ya Mtume (s.a.w.w): “من كنت مولاه فهذا علي مولاه” Ushuhuda wa Masahaba waliompongeza Imam Ali (a.s). Tofauti kati ya pongezi hizo na matendo yao baada ya kufariki Mtume (s.a.w.w).
Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA-Jamiat Al-Mustafa (s) - Tawi la Dar-es-Salaam - Tanzania, imefanya Kongamano la Kielimu kuhusiana na Dakika za Mwisho za Uhai wa Bwana Mtume (saww) na Kuchunguza Matukio kadhaa na Muhimu yaliyojiri karibia na Mwisho wa Maisha yake (s.a.w.w) ya hapa Duniani. Miongoni mwa Matukio Muhimu yaliyojiri karibia na Mauti ya Mtume (s.a.w.w), ni pamoja na Tukio la Hijjatul Widaa.
Hijja hiyo imeitwa "Hijja ya Kuaga" kwa sababu Mtume (s.a.w.w) aliitumia kuwaaga Waislamu, na kuwaaga Waumini, na kuwaaga watu wote kwa ujumla.
Ni Hijja iliyo fanyika mwaka wa 10 Hijria, na baada ya Tukio la Fat'hu Makkah lililojiri mwaka wa 8 Hijria. Na baada ya Hijja hii ya Kuaga, ilipita Miezi mitatu, kisha Mtume (s.a.w.w) akaaga Dunia, na ilikuwa Siku ya Jumatatu, tarehe 28 Mwezi wa Safar.
Mtume (s.a.w.w) aliitumia Hijjatul Widaa kuwausia Mengi Waislamu yanayohusiana na Dini yao Tukufu ya Kiislamu. Na miongoni mwa hayo ni pamoja na kusisitiza juu ya Maadili Mema ya Kidini kama vile:
1_Msisitizo juu ya udugu baina ya Waumini, kwamba Waislamu wanatakiwa kuishi kwa upendo na maelewano na Ushirikiano kwa sababu Waumini ni ndugu kama Qur'an Tukufu ilivyo sema.
2_Msisitizo juu ya Umoja wa Kiislamu. Kwamba Waislamu Dini yao ni moja na Quran yao ni moja na Mtume wao ni mmoja, hivyo ili wawe na Nguvu kama Waislamu na wailinde heshima yao, wanatakiwa kuishi kwa kuungana na kushikamana na kudumisha Umoja wao.
3_Alisisitiza juu ya ufuataji wa Qur'an Tukufu na Ahlul-Bayt wake (as) kwamba viwili hivi ndio Nguzo Kuu, na ni Vizito viwili vitakavyouongoza Umma wa Kiislamu baada yake (s.a.w.w).
Na katika msisitizo huo, tunapata Tangazo la Wilayat ambapo Mtume (s.a.w.w) aliitumia Hijjatul Widaa kutangaza Wilayat ya Amirul Muuminina, Ali bin Abi Talib (as), pindi alipotangaza katika Siku ya Ghadir tarehe 18 Dhilhijja kwamba:
"من كنت مولاه فهذا علي مولاه"
"Yeyote niliyekuwa Maula / Kiongozi wake, basi huyu Ali ni Maula / Kiongozi wake".
Alitumia fursa kutangaza hilo wazi wazi kwa Umma wenye kusikia kwa masikio yao na kuona kwa macho kwamba mjue kuwa baada yangu Khalifa wenu ni Ali bin Abi Talib (as).
Masahaba Wote waliohudhuria katika Hujjatul Widaa, katika eneo la bonde la Ghadir, walijitokeza mmoja mmoja kumpongeza Ali bin Abi Talib (as) kuwa: "Hongera Hongera Ewe Mwana wa Abu Talib, Leo hii imekuwa Maula / Kiongozi wangu na Kiongozi wa kila Muislamu Mwanaume na Mwanamke".
Lakini kwa Bahati mbaya Sana, baadhi ya waliompongeza Siku hiyo mbele za Mtume (s.a.w.w), ndio waliokuwa mstari wa mbele kujivisha Vazi la Ukhalifa baada ya Uhai wa Bwana Mtume (s.a.w.w)!.
Matukio ya kabla ya Uhai wa Mtume (saww) ni Mengi mno, yapo mazuri ya kufurahisha na yapo yenye kutia machungu na Kusikitisha.
Moja ya Matukio yanayosikitisha yaliyotokea karibia na Uhai wa Mtume wetu Muhammad (s.a.w.w) ni jaribio la kumuua kwa Sumu. Jaribio hili kilifanywa na Mwanamke wa Kiyahudi aliyeitwa Zainab Binti Ha'rithi, ili kulipiza Kisasi Kwa niaba ya ndugu na Jamaa zake wa Kiyahudi waliouliwa Siku ya vita vya Khaibar.
Alimtilia Sumu Mtume Muhammad (s.a.w.w) katika chakula, na ikamsumbua na kupelekea maradhi ya Mtume (s.a.w.w). Na ndio maana katika baadhi ya riwaya inatajwa kuwa Mtume (s.a.w.w) alikufa Shahidi, kama walivyo wengi katika Kizazi chake Kitukufu waliouliwa na wakafa Kishahidi, ukianzia kwa Binti yake Kipenzi Sayyidat Fatima (sa), Ali bin Abi Talib (as), na wajukuu zake ambao ni Maimam na Makhalifa katika mlolongo wa Makhalifa halali na Sahihi Kumi na Wawili, idadi ambayo ni kwa mujibu wa kauli na maelekezo ya mwenyewe Mtume Muhammad (s.a.w.w).
Mpaka Mtume wetu Muhammad (saww) anafariki, mtu aliyekuwa Karibu mno na Mtume (saww) ni Imam Ali bin Abi Talib (as). Wakati Roho Tukufu ya Mtume Muhammad (saww) inatolewa na kutenganishwa na kiwili wili chake, Imam Ali (as) alikuwa amemkumbatia Mtume (saww) na Kichwa chake kimelala juu ya kifua chake.
Na hakuna mtu aliyekuwa Karibu zaidi na Mtume (s.a.w.w) katika Uhai wake na baada ya Mauti yake kuliko Imam Ali bin Abi Talib (as).
Your Comment