Sheikh Dkt. Saleh Maulid kuhusiana na Nafasi ya kielimu ya Imam Ridha (a.s) alibainisha namna Imam alivyoshiriki katika mijadala ya kielimu na kihistoria katika zama za Abbasiyya, na mchango wake mkubwa katika kuimarisha hoja za Kiislamu mbele ya wajuzi na wanazuoni wa nyakati zake".
Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Leo hii, Tarehe 23 Agosti 2025 - Jumamosi - Kwa heshima ya kumbukumbu ya Shahada ya Imam Ali bin Musa al-Ridha (a.s), Waumini na Wapenzi wa Ahlul-Bayt (a.s) wamekusanyika katika kikao maalum kilichoambatana na kisomo cha Dua ya Nudba, dua mashuhuri ya maombolezo na matumaini ya kuungana na Imam wa Zama (a.t.f.s).
Katika maadhimisho haya, mgeni rasmi na mzungumzaji wa siku hiyo alikuwa Haji Dkt. Saleh Maulid, ambaye alitoa hotuba yenye maudhui ya kielimu na kiroho kuhusu nafasi ya Imam Ridha (a.s) katika kuimarisha imani na kueneza elimu ya dini katika Ulimwengu wa Kiislamu.
Katika maelezo yake, Dkt. Saleh Maulid alifafanua kwa kina:
- Nafasi ya kielimu ya Imam Ridha (a.s): Alibainisha namna Imam alivyoshiriki katika mijadala ya kielimu na kihistoria katika zama za Abbasiyya, na mchango wake mkubwa katika kuimarisha hoja za Kiislamu mbele ya wajuzi na wanazuoni wa nyakati zake.
- Uimarishaji wa Imani: Alieleza jinsi Imam Ridha (a.s) alivyojenga ngome thabiti ya kiimani katika nyoyo za Waislamu kupitia mafundisho yake, tabia zake na mawasiliano yake ya karibu na wafuasi wake.
- Mchango wa Kiutamaduni na Kimaadili: Imam Ridha (a.s) alikuwa ni mfano bora wa huruma, ukarimu na hekima, sifa ambazo zimeendelea kuwa urithi na dira ya kielimu na kiroho hadi leo.
-
Washiriki wa kikao hicho walionekana kuguswa na maudhui ya hotuba na kusisitiza kuwa kumbukumbu ya Imam Ridha (a.s) inabeba somo kubwa la kuimarisha mshikamano wa kidini na kudumisha uhusiano wa dhati na Ahlul-Bayt (a.s).
Sheikh Saleh Maulid alitumia fursa hiyo kuhimiza Waumini kuendelea kushikamana na mafundisho ya Imam Ridha (a.s) kwa kuwa ndiyo njia bora ya kuimarisha imani na kukabiliana na changamoto za kiroho, kijamii na kitamaduni katika zama hizi.
Your Comment