Sheikh Muhammad Abdu: “Mtume wetu Muhammad (s.a.w.w) alikuwa mfano bora wa kuwaenzi wanawake na kuwapa nafasi ya msingi katika jamii. Ni juu yetu kufuata nyayo zake kwa kuendeleza elimu, maadili na heshima kwa wanawake katika Uislamu"
Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Dar es Salaam - Tanzania, Katika kuadhimisha Maulidi ya Mtume Muhammad (s.a.w.w), Kitengo cha Wanawake cha Jumuiya ya Shia Ithna Ashari Tanzania (T.I.C) leo hii tarehe 06-09-2025, kimeandaa hafla maalum ya Maulid ya Kuzaliwa kwa Mtume wa Rehma, Sayyidul Anbiyaa wal-Mursalimina, Muhammad (s.a.w.w) iliyofanyika katika Masjid Ghadir, Kigogo Post, Jijini Dar es Salaam, Tanzania.
Hafla hiyo adhimu imehudhuriwa na wageni mbalimbali kutoka ndani na nje ya jiji la Dar es Salaam, wakiwemo wanachama wa jumuiya, viongozi wa dini, na wawakilishi kutoka taasisi mbalimbali za Kiislamu.
Miongoni mwa wageni mashuhuri waliotoa hotuba katika Hafla hiyo ni Samahat Sheikh Muhammad Abdu, Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini ya T.I.C na Naibu Mudir wa Hawzah Imam Sadiq (a.s). Katika hotuba yake, Sheikh Muhammad Abdu alitoa nasaha muhimu kwa wanawake wa Kiislamu, akiangazia jukumu la mwanamke mwenye imani katika kueneza elimu na maarifa ya Kiislamu, kwa kuongozwa na mafundisho ya Mtume Muhammad (s.a.w.w).
“Mtume wetu Muhammad (s.a.w.w) alikuwa mfano bora wa kuwaenzi wanawake na kuwapa nafasi ya msingi katika jamii. Ni juu yetu kufuata nyayo zake kwa kuendeleza elimu, maadili na heshima kwa wanawake katika Uislamu,” alisema Sheikh Muhammad Abdu.
Katika hotuba hiyo, alisisitiza umuhimu wa wanawake wa Kiislamu kuwa nguzo za maarifa, malezi ya kiroho, na ujenzi wa jamii zenye misingi ya tauhidi na maadili bora. Alieleza kuwa maulidi haya yanapaswa kuwa chachu ya kuongeza mapenzi ya dhati kwa Mtume (s.a.w.w) na utekelezaji wa mafundisho yake katika maisha ya kila siku.
Hafla hii ya kipekee pia ilihusisha qaswida, burdah na mijadala ya kielimu iliyoandaliwa na wanawake wenyewe, ikionyesha ushiriki mkubwa wa wanawake katika kusherehekea na kuenzi kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Rehma kwa walimwengu wote.
Kwa ujumla:
Hafla hii imedhihirisha kwa mara nyingine kuwa wanawake wa Jumuiya ya Shia Ithna Ashari Tanzania wana nafasi muhimu katika kuendeleza harakati za kielimu, kiroho, na kijamii kwa kuongozwa na nuru ya Mtume Muhammad (s.a.w.w) na Ahlul-Bayt wake watoharifu (a.s).
Your Comment