Hafla Kubwa Ya Kumbukumbu Za Kuzaliwa Mtume Muhammad (SAW) na Imam Ja'far Sadiq (AS) Yazikutanisha Wataalamu na Wageni Wapatao 1500 Dar-es-Salaam.Hafla hii imekuwa ni fursa muhimu ya kuimarisha uelewa wa maisha ya Mtume Muhammad (s.a.w.w) na mafanikio ya Imam Ja'far Sadiq (AS) pamoja na kuhamasisha Umoja baina ya Waislamu na Heshima kwa Wanawake katika jamii zetu.
Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Leo tarehe 7 -09 - 2025, hafla muhimu ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Mtume Mtukufu Muhammad (s.a.w.w) pamoja na Imam Ja'far Sadiq (a.s) imefanyika kwa mafanikio makubwa katika Madrasa ya Hazrat Zainab (sa), iliyoko Jijini Dar-es-Salaam, Tanzania. Hafla hii imeandaliwa na Uwakilishi wa Jamiat al-Mustafa (SA) Tanzania, chini ya Uongozi na Usimamizi wa Dr.Ali Taqavi.
Zaidi ya wageni 1500 walihudhuria katika tukio hili, ikiwa ni pamoja na Masheikh, Wasomi, Walimu, Wanafunzi na watu mashuhuri kutoka taasisi mbalimbali za Kiislamu, Kiserikali na binafsi.
Mgeni rasmi wa hafla hii alikuwa ni: Samahat Sheikh Dr. Alhad Mussa Salum, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT-TAIFA), ambaye alitoa hotuba ya kipekee na maridhawa kuhusu maisha na mafanikio ya Mtume Muhammad (s.a.w.w).
Katika hotuba yake, Sheikh Dr. Alhad Mussa Salum alisisitiza jinsi Mtume Muhammad (s.a.w.w) alivyoleta Uislamu wenye kuzingatia heshima kubwa kwa Mwanamke, akionyesha kuwa kabla ya kuja kwa Uislamu, Wanawake walikumbwa na unyanyasaji na udhalilishaji mkubwa, kiasi kwamba wengine walikuwa wakizikwa wakiwa hai, kosa lao likiwa ni kuzaliwa Wanawake!.
"Mwanamke ni kiumbe muhimu sana anayetakiwa kuheshimiwa katika jamii," aliongeza Sheikh Dr.Alhad, akisisitiza kwamba heshima hii ni lazima ilindwe kwa kila wakati.
Alibainisha kuwa leo hii, jamii zinapaswa kupinga mila na tabia zinazoendelea kumdhalilisha Mwanamke, kama vile matumizi ya midoli katika biashara - yenye sura na taswira ya Mwanamke - isiyo na heshima kwa Mwanamke.
Aliongeza na kupendekeza kuwa ni muhimu katika biashara hizo zinazotumia Midoli yenye Taswira ya Mwanamke, kuweka kanuni za kimaadili na za kijamii katika matumizi ya Midoli hiyo ili kuhifadhi heshima ya Mwanamke.
Hafla hii imekuwa ni fursa muhimu ya kuimarisha uelewa wa maisha ya Mtume Muhammad (s.a.w.w) na mafanikio ya Imam Ja'far Sadiq (AS) pamoja na kuhamasisha Umoja baina ya Waislamu na Heshima kwa Wanawake katika jamii zetu.
Your Comment