"Mtume wa Amani - Uchaguzi Uwe wa Haki, Demokrasia na Amani"
Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Dar es Salaam, 2025 / 1447 H – Jumuiya ya Shia Ithna’ashariyyah Tanzania (T.I.C) imeandaa Zafa maalum ya kusherehekea Maulid ya kuzaliwa kwa Mtume wa mwisho wa Mwenyezi Mungu, Mtume Muhammad Al-Mustafa (S.A.W.W), katika eneo la Kigogo Post, jijini Dar es Salaam.
Maadhimisho haya yamefanyika kwa hali ya amani, mshikamano na mapenzi makubwa kwa Mtume wa Uislamu, yakiambatana na maandamano ya Amani (Zafa), nyimbo za kaswida, salawat, na hotuba mbalimbali zinazotilia mkazo juu ya sira njema ya Mtume (S.A.W.W).
Kaulimbiu ya Tukio:
"Mtume wa Amani - Uchaguzi Uwe wa Haki, Demokrasia na Amani."
Kaulimbiu hii imekusudia kuunganisha mafundisho ya Mtume Muhammad (S.A.W.W) na mazingira ya sasa ya kijamii na kisiasa, ikihimiza umuhimu wa haki, uadilifu, na mshikamano wa kitaifa katika kipindi muhimu cha uchaguzi.
Sherehe hii imeambatana na ujumbe wa umoja, ambapo kauli mbiu ndogo: "Kitabu_Kimoja, Mtume_Mmoja na Umma_mmoja" zilitumika kuhamasisha mshikamano miongoni mwa Waislamu wote na kuhimiza urejeo kwa Qur'an, Sira ya Mtume na Umoja wa Umma wa Kiislamu.
Wakati wa Zafa, waumini walibeba mabango ya amani, walikumbusha sifa za rehema za Mtume (S.A.W.W) na kutoa wito kwa jamii nzima kuhakikisha uchaguzi mkuu ujao unaendeshwa kwa misingi ya haki, amani na utulivu.
Your Comment