Samahat Sheikh Dr. Abdur-razak Amir Msuya, Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT-TAIFA), katika Hafla Tuzo za Kielimu za Mufti (Mufti Education Awards) aliibuka mshindi wa "Tuzo Bora ya Uandishi Katika Elimu ya Kiislamu". Tuzo hiyo imetambua mchango wake mkubwa katika kuandika na kueneza maudhui yenye kuelimisha na kujenga jamii kwa misingi ya Kiislamu.
Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Dar es Salaam, Tanzania – Kwa mara ya kwanza katika historia, hafla ya tuzo za kipekee za kielimu zilizojulikana kama "Mufti Education Awards" | "Tuzo za Kielimu za Mufti" ilifanyika katika Ukumbi wa Serena Hotel Jijini Dar es Salaam. Tukio hili, lililoadhimishwa kwa Kutambuliwa kama “Mufti Day”, limefahamika rasmi kama jukwaa muhimu la kuthamini elimu na maarifa katika jamii ya Kitanzania.
Mgeni rasmi wa hafla hiyo alikuwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye aliwakilishwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa.
Katika tuzo hizo, wadau mbalimbali waliotambulika kwa juhudi zao za kueneza elimu na maarifa walipongezwa na kutuzwa kwa mchango wao mkubwa katika kukuza maendeleo ya elimu nchini.
Tuzo kubwa ya kwanza ilikwenda kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutambua mchango wake mkubwa katika kuhimiza na kusimamia maendeleo ya elimu Tanzania.
Miongoni mwa washindi waliotunukiwa tuzo ni Samahat Sheikh Dr. Abdur-razak Amir Msuya, Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT-TAIFA), ambaye alibuka na Tuzo Bora ya Uandishi Katika Elimu ya Kiislamu. Tuzo hiyo imetambua mchango wake mkubwa katika kuandika na kueneza maudhui yenye kuelimisha na kujenga jamii kwa misingi ya Kiislamu.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mufti Mkuu wa Tanzania, Sheikh Dr. Abubakar Zubair bin Ally, alisisitiza umuhimu wa elimu katika Uislamu, akisema:
“Tuzo hizi zina lengo la kudhihirisha ukweli halisi wa Uislamu kuhusiana na elimu kwamba Uislamu ni dini ya elimu na maarifa, inayopiga vita ujinga. Mtu yeyote anayethamini elimu, anastahili kuthaminiwa na kupongezwa.”
Kwa ujumla, tukio hili limeweka alama muhimu katika historia ya elimu nchini Tanzania, likionesha dhamira ya dhati ya viongozi wa dini na serikali katika kushirikiana kukuza elimu na maarifa kwa manufaa ya taifa.
Your Comment