Sheikh Dr. Al-Had Mussa Salum pia ametoa wito wa kuepuka maandamano na matendo yoyote yanayoweza kuvuruga amani ya nchi, akitahadharisha kuhusu taarifa za tishio la maandamano yaliyopangwa kufanyika tarehe 29. “Nina uhakika Watanzania ni watu wenye busara; hawawezi kuingizwa katika maandamano yasiyo na faida. Hakuna kijana wa Kiislamu atakayethubutu kushiriki katika jambo litakalomletea madhara bila kupigania dini yake,”
Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Dar es Salaam - Tanzania, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT-TAIFA), Sheikh Dr. Alhad Mussa Salum, ameeleza kwa ufafanuzi mpana maana ya Tasawuf (Usufi), akibainisha kwamba kiini cha Tasawuf ni adabu, utiifu, na tabia njema (Akhlaq).
Amesema kuwa katika mafundisho ya Twariqa, murid (mfuasi) anatakiwa kuwa Mtiifu kwa Sheikh wake na kwa Makhalifa, kwani nafasi ya Masheikh mbele ya wanafunzi wao ni sawa na nafasi ya Mtume mbele ya Umma wake. “Hivyo ndivyo murid wa kweli anavyokuwa,” amesema Sheikh Dr. Mussa Salum.
Ushiriki wa Waislamu Katika Uchaguzi
Akiwa anazungumzia kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Tanzania, Sheikh Dr. Mussa Salum amewataka wanatwariqa na Waislamu wote kushiriki ipasavyo katika mchakato huo, akisema:
“Katika Uislamu inajuzu kwa Muislamu kushiriki katika uchaguzi kwa hoja za kiakili na za kunakili; wala si haramu kwake kushiriki. Dalili za uhalali wa kupiga kura katika nchi kama Tanzania zipo nyingi na za kutosha.”
Ameongeza kuwa ni wajibu wa Waislamu kufuata maelekezo ya viongozi wa dini na taasisi husika, pamoja na taratibu zilizowekwa na Tume ya Uchaguzi, ili kuhakikisha zoezi la uchaguzi linafanyika kwa amani, nidhamu na utulivu.
“Baada ya kupiga kura, tuwaachie wahusika wasimamie kwa mujibu wa taratibu zilizopo. Kazi ya Muislamu ni kushiriki kwa amani, si kulinda kura kwa fujo,” alisisitiza Sheikh Dr. Mussa Salum.
Kukataa Vurugu na Maandamano
Sheikh Dr. Mussa Salum pia ametoa wito wa kuepuka maandamano na matendo yoyote yanayoweza kuvuruga amani ya nchi, akitahadharisha kuhusu taarifa za tishio la maandamano yaliyopangwa kufanyika tarehe 29.
“Nina uhakika Watanzania ni watu wenye busara; hawawezi kuingizwa katika maandamano yasiyo na faida. Hakuna kijana wa Kiislamu atakayethubutu kushiriki katika jambo litakalomletea madhara bila kupigania dini yake,” amesema.
Amesisitiza kuwa viongozi wa dini zote nchini wanahimiza amani na utulivu, na hivyo ni jukumu la kila raia kushiriki katika uchaguzi kwa njia ya kistaarabu.
Tasawuf ni Njia ya Amani
Kwa kumalizia, Sheikh Dr. Mussa Salum amesema kuwa Tasawuf ya kweli humpeleka mtu katika amani, upole na utiifu kwa mamlaka halali.
“Usufi unatuongoza tupige kura kwa utulivu, bila fujo wala chuki. Hiyo ndiyo Tasawuf - kuwa mtu wa amani, maelewano na utiifu,” amehitimisha.
-
Imeandaliwa na Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA-
Your Comment