Mufti: “Tunaizungumzia amani na uzalendo kwa sababu tunajua umuhimu wake katika Taifa. Wapo wanaodhani sisi ni vibaraka wa Serikali - hapana! Hatutumwi na Serikali. Tunatambua wajibu wetu wa kuisaidia jamii kuelewa maana ya kuwa mzalendo wa kweli,”
Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Sheikh Dr. Abubakar Zubeir bin Ally, amesisitiza kuwa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) halitumiki na Serikali bali linafanya kazi kwa ajili ya maslahi ya Taifa, likihimiza amani, umoja, na uzalendo miongoni mwa Watanzania.
Mheshimiwa Mufti, Sheikh Dr. Abubakar Zubeir bin Ally, aliendelea kubainisha na kuweka mambo wazi akisema kwamba Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) litaendelea kutekeleza wajibu wake wa kusimamia maslahi ya Taifa kwa kuhimiza amani, umoja, na mshikamano wa kijamii.
Alitoa kauli hiyo leo, Oktoba 10, 2025, wakati wa ziara yake ya kikazi Mkoani Njombe, alipokutana na baadhi ya viongozi wa Dini na Serikali katika kikao cha mashauriano kuhusu hali ya amani nchini.
Mufti Mkuu, Dkt.Abubakar Zubeir amesema kuhusiana na baadhi ya watu kwamba wamekuwa wakidhani kimakosa kuwa Baraza hilo linatumiwa na Serikali, jambo ambalo amelikataa vikali, akisisitiza kuwa misimamo ya BAKWATA imejengwa juu ya msingi wa uzalendo, uadilifu, na maslahi mapana ya Watanzania.
“Tunaizungumzia Amani na uzalendo kwa sababu tunajua umuhimu wake katika Taifa. Wapo wanaodhani sisi ni vibaraka wa Serikali - hapana! Hatutumwi na Serikali. Tunatambua wajibu wetu wa kuisaidia jamii kuelewa maana ya kuwa mzalendo wa kweli,” alisema Mufti Mkuu wa Tanzania Dkt.Abubakar Zubeir bin Ally.
Aidha, alihimiza viongozi wa Dini na Wananchi wote kudumisha amani na upendo, akibainisha kuwa maendeleo ya Taifa hayatawezekana pasipo umoja na mshikamano.
Your Comment