Shule ya Imam Ali (a.s) Secondary School Girls - Arusha, inatambulika kwa mfanano wake wa kielimu na kimaadili, ikitoa elimu bora inayochanganya masomo ya kisekula na mafundisho ya dini ya Kiislamu kwa misingi na mienendo ya Ahlul-Bayt (a.s).
Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt as -ABNA- Arusha, Tanzania - Jumatatu, tarehe 13 Oktoba 2025 - Sheikh Mkuu wa Jumuiya ya Shia Tanzania (TIC), Maulana Sheikh Hemed Jalala Mwakindenge, akiwa katika ziara yake ya kikazi Mkoani Arusha, amepata fursa ya kutembelea Shule ya Sekondari ya Imam Ali (a.s) kwa Wasichana, iliyo chini ya usimamizi wa Samahat Sheikh Maulid Sombi.
Ziara hiyo ililenga kukagua maendeleo ya kielimu na kiimani ya Wanafunzi, pamoja na kuimarisha uhusiano wa kiutendaji kati ya taasisi za elimu za Kiislamu na Uongozi Mkuu wa Jumuiya ya Shia Tanzania (TIC).
Katika hotuba yake fupi kwa walimu na wanafunzi wa shule hiyo, Sheikh H. Jalala alisisitiza umuhimu wa elimu yenye maadili, akisema kuwa:
"Elimu bora ni ile inayomjenga mwanafunzi kielimu na kiroho, ikimfanya awe mtiifu kwa Mwenyezi Mungu na mwenye manufaa kwa jamii".
Aidha, alitoa pongezi maalum kwa Samahat Sheikh Maulid Sombi kwa juhudi zake kubwa katika kuendeleza elimu ya Kiislamu, hususan kwa wasichana, na kuhakikisha mazingira ya kujifunzia yanakuwa ya kimaadili, salama na yenye kuhamasisha tafakuri ya kiimani.
Kwa upande wake, Sheikh Maulid Sombi alimshukuru Sheikh Mkuu kwa heshima ya kutembelea shule hiyo, akieleza kuwa ziara hiyo ni ishara ya Umoja na Mshikamano wa Viongozi wa Kiislamu nchini, na ni motisha kubwa kwa walimu na wanafunzi kuendelea kufanya vizuri zaidi katika masomo na mwenendo Safi wa kidini.
Shule ya Imam Ali (a.s) Secondary School Girls - Arusha, inatambulika kwa mfanano wake wa kielimu na kimaadili, ikitoa elimu bora inayochanganya masomo ya kisekula na mafundisho ya dini ya Kiislamu kwa misingi na mienendo ya Ahlul-Bayt (a.s).
Ziara hiyo ilihitimishwa kwa dua ya pamoja na mawaidha mafupi, yakihimiza amani, uadilifu, na bidii katika kusoma na kufundisha kwa ajili ya kupata radhi za Mwenyezi Mungu.
Your Comment