Sheikh Hemed Jalala Katika Hotuba yake aliwahimiza Waislamu Duniani kote, hususan vijana na Wanazuoni, kuutafakari kwa kina "Ustaarabu wa Kiislamu" na kuutumia kama dira ya maendeleo endelevu. Alisisitiza kuwa ustaarabu huu unatoa suluhisho kamili kwa changamoto za kisasa - kuanzia maadili, siasa, uchumi hadi ustawi wa jamii.
Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt as -ABNA- Dar es Salaam, Tanzania - 16 Oktoba 2025 Sheikh Mkuu wa Jumuiya ya Shia Ithnaasharia Tanzania (TIC), Maulana Sheikh Hemed Jalala Mwakingende, ameshiriki katika Kikao Maalumu cha Kiutafiti na Kisayansi kilichojikita katika mada ya “Misingi ya Ustaarabu wa Kimagharibi katika Kuukoloni Ulimwengu kwa Mujibu wa Fikra na Mtazamo wa Sayyid Ali Khamenei (H.A)”.
Kikao hicho kimefanyika leo (Alkhamisi) katika Chuo cha Jamiat al-Mustafa (s) kilichopo Mbezi Beach, Dar es Salaam - Tanzania, chini ya usimamizi na uongozi wa Hujjatul Islam, Dr. Ali Taqavi, na kupitia Kitengo cha uratibu wa masuala ya kielimu na Kiutafiti cha Jamiat Al-Mustafa (s), Kikiongozwa na Samahat Sheikh Dr.Reihan Yasin.
Mada Kuu na Uchangiaji wa Sheikh H.Jalala
Katika kikao hicho, Maulana Sheikh Hemed Jalala aliwasilisha uchambuzi wa kina wa mada yenye kichwa: “Muundo wa Ustaarabu wa Kimagharibi na Namna ya Kuufahamu.”
Katika maelezo yake, Sheikh Jalala alifafanua historia ya kuzaliwa kwa ustaarabu wa Kimagharibi, misingi yake ya kifikra, pamoja na namna ulivyokuwa chombo cha kuendeleza sera za ukoloni na ubinafsi katika nyanja mbalimbali za maisha ya Binadamu.
Alibainisha kuwa ustaarabu wa Kimagharibi umejengwa juu ya misingi ya ufasihi wa kimaada, ubinafsi, na utawala wa nguvu, Ukandamizaji, tofauti kabisa na ustaarabu wa Kiislamu aliyokuja Mtume wetu Muhammad (saww) unaojikita katika maadili, uadilifu, haki, utu, na kumtumikia Mwanadamu kwa misingi ya Tauhidi.
Sheikh Jalala pia aliweka bayana umuhimu wa kuelewa tofauti hizi ili Waislamu waweze kuendeleza ustaarabu wao wa kipekee unaotegemea misingi ya Qur’an Tukufu na Sunna za Mtume (s.a.w.w).
Mahudhurio na Faida za Kielimu
Kikao hicho kilihudhuriwa na wanafunzi wa elimu ya juu ya Kiislamu, wahadhiri, pamoja na viongozi wa taasisi mbalimbali za Kiislamu nchini Tanzania. Washiriki walinufaika kwa kiwango kikubwa kupitia mijadala na tafiti zilizowasilishwa, ambazo ziliangazia mtazamo wa Sayyid Ali Khamenei (H.A) kuhusu uhalisia wa ustaarabu wa Kimagharibi na athari zake katika jamii za ulimwengu wa tatu.
Washiriki wengi walipongeza mchango wa Sheikh Hemed Jalala kwa uchambuzi wake wa kina, wenye mifano hai, kinaishi, na uwezo wake wa kulinganisha ustaarabu wa Kiislamu na ule wa Kimagharibi kwa njia iliyoeleweka kwa hadhira na ya kielimu.
Kielelezo cha Ustaarabu Hai wa Kiislamu
Katika maelezo yake, Maulana Sheikh Jalala aliwakumbusha washiriki kuhusu mfano wa kihistoria wa Marhumu Imam Ayatollah Ruhullah Khomeini (M.A), aliyelitangaza na kulisimamisha Ustaarabu wa Kiislamu kwa vitendo kupitia mapinduzi ya mwaka 1979 yaliyozaa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Alibainisha kuwa, kupitia juhudi za Imam Khomeini, ulimwengu uliona taifa lililosimama imara katika kulinda heshima na utu wa kila mwanadamu, bila kujali dini, dhehebu, kabila, au rangi. “Sheikh Jalala alisema kuwa misingi hii mizuri ya Kiislamu ndiyo iliyozalisha jamii inayotanguliza haki, uadilifu, na utu, misingi ambayo hadi leo inaendelezwa kwa hekima na uthabiti na Sayyid Ali Khamenei (Allah Amuhifadhi kwa ajili ya Uislamu na Waislamu),” aliongeza.
Wito wa Kuendeleza Ustaarabu wa Kiislamu
Sheikh H. Jalala aliwahimiza Waislamu duniani kote, hususan vijana na Wanazuoni, kuutafakari kwa kina Ustaarabu wa Kiislamu na kuutumia kama dira ya maendeleo endelevu. Alisisitiza kuwa ustaarabu huu unatoa suluhisho kamili kwa changamoto za kisasa - kuanzia maadili, siasa, uchumi hadi ustawi wa jamii.
Kwa mujibu wake, “Kuendelea kushikamana na utamaduni na ustaarabu wa Kiislamu ni kuendelea kulinda utu wa Mwanadamu na kuendeleza Amani ya kweli katika dunia”.
Kiujumla: Kikao hiki cha kiutafiti kimekuwa ni fursa adhimu ya kubadilishana maarifa, kukuza fikra za kiutamaduni, na kuhimiza mwelekeo wa kielimu unaojikita katika kujenga ustaarabu wa Kiislamu unaoweza kukabiliana na changamoto za ustaarabu wa Kimagharibi katika zama hizi.
Your Comment