Mufti Mkuu alitoa wito maalum kwa wanasiasa na wananchi wote katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi, kuendelea kulinda amani, kuepuka maneno ya chuki na kuhakikisha Tanzania inabaki kuwa nchi ya utulivu na maridhiano.
Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Dar es Salaam, Tanzania - Maulid ya Mtume (saww) (Masjid Majmuuat Al-Islamiyya) imekuwa Maulid ya viwango vya juu, yenye ubunifu wa hali ya juu na kukusanya sifa zote njema za ubora na mafanikio, lakini pia imekuwa ni Maulid ya Upendo, Umoja na Mshikamano, ambapo imefanyika Siku ya Ijumaa (17-10-2025) katika Viwanja vya Masjid Majmuuat Al-Islamiyya, Temeke Mwisho.
Hafla hiyo adhimu ilihusisha Ushiriki mkubwa wa Waumini na Viongozi wa Dini na Serikali kutoka sehemu mbalimbali za nchi, ikiongozwa na Imam Mkuu wa Masjid hiyo, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT-TAIFA), Sheikh Dkt. Alhad Mussa Salum.
Mgeni rasmi wa hafla hiyo alikuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa, aliyewakilishwa na Mufti Mkuu wa Tanzania, Sheikh Dr. Abubakar Zubair bin Ally.
Katika hotuba yake, Mufti Mkuu wa Tanzania alisema:
"Hadhara hii ya Maulid Tukufu katika viwanja hivi mara nyingi huihesabu kama hadhara yangu binafsi, lakini leo niko hapa kumwakilisha Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kasim Majaliwa, ambaye anawapongeza sana Waumini na watu wote kwa kuhudhuria katika tukio hili adhimu, na kumpongeza zaidi Sheikh Dkt. Alhad Mussa Salum kwa uongozi wake, uratibu wake na usimamizi wa Maulid haya."
Akiwasilisha salamu za Waziri Mkuu, Mufti Mkuu alisisitiza kuwa Amani ni nguzo kuu inayopaswa kuzungumzwa na kuenziwa zaidi katika kipindi hiki.
“Mheshimiwa Waziri Mkuu amenituma kusisitiza umuhimu wa Amani, kwani hakuna jambo muhimu zaidi kwa taifa letu kwa sasa kama kuzungumzia na kulinda Amani yetu,” alisema Mufti Mkuu.
Katika sehemu ya pili ya hotuba yake, Sheikh Dr. Abubakar alichambua kwa kina Umuhimu wa Amani kwa mujibu wa mafundisho ya Kiislamu, akibainisha kuwa Amani ni zawadi kubwa ya Mwenyezi Mungu kwa Mwanadamu, na hata Pepo yenyewe imeelezewa kama Makao ya Amani:
“Mwenyezi Mungu amesema: ‘Ingieni Peponi kwa Amani.’ Hili linaonesha kuwa Amani ndiyo hali ya juu kabisa ambayo Mwenyezi Mungu amewaandalia waja wake wema.”
Mufti Mkuu alitoa wito maalum kwa wanasiasa na wananchi wote katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi, kuendelea kulinda amani, kuepuka maneno ya chuki na kuhakikisha Tanzania inabaki kuwa nchi ya utulivu na maridhiano.
“Tuidumishe Amani yetu, tusikubali mtu yeyote aitikise au aivuruge. Amani ni tunu, ni zawadi ya Mwenyezi Mungu kwetu sote,” alihitimisha.
Tukio hilo lilipambwa na qaswida, mawaidha ya kielimu, na hotuba za kuenzi maisha na mafunzo ya Mtume Muhammad (s.a.w.w), yakibeba ujumbe wa elimu, maadili, na uhuishaji wa mapenzi kwa Mtume wa Rehema.
Your Comment