Maulid hayo yamehitimishwa kwa dua maalum ya kuombea umoja wa Waislamu, amani ya taifa na ustawi wa jamii, sambamba na pongezi kwa waandaaji wote waliowezesha kufanyika kwa hafla hiyo kwa mafanikio makubwa.
Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (a.s) - ABNA-
Kwa furaha, heshima na mapenzi makubwa kwa Mtume wa Uislamu, Muhammad Mustafa (s.a.w.w), Waislamu wa madhehebu mbalimbali, hususan wafuasi wa Ahlul-Bayt (a.s), wameungana katika Maulid ya kuzaliwa kwa Mtume Mtukufu yaliyofanyika katika Kituo cha Bilal Moshi, mkoani Kilimanjaro - Tanzania.
Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi wa dini na taasisi za Kiislamu, wanazuoni, waumini, pamoja na vijana na wanawake kutoka maeneo mbalimbali ya mkoa huo. Maulid haya yamekuwa jukwaa la kuhuisha mapenzi, umoja na mafunzo yanayotokana na maisha bora ya Mtume Muhammad (s.a.w.w) - kigezo cha rehema, haki na amani kwa ulimwengu mzima.
Katika hafla hiyo, wahadhiri na masheikh mashuhuri walitoa hotuba zilizosisitiza umuhimu wa kuiga tabia, maadili na mwanga wa Mtume (s.a.w.w) katika kujenga jamii yenye upendo, mshikamano na uadilifu. Aidha, zilisomwa qaswida, mashairi na tenzi za kumsifu Mtume Mtukufu, huku waumini wakijawa na furaha na hisia za kiroho.
Viongozi wa Bilal Moshi walisema kuwa tukio hilo si tu sherehe ya kuzaliwa kwa Mtume, bali ni fursa ya kuhuisha utajo wake, kufundisha maadili yake, na kuimarisha umoja wa Kiislamu unaozingatia mafundisho ya Qur’ani na Sunna sahihi.
Aidha, wamesisitiza kuwa katika kipindi hiki cha changamoto mbalimbali duniani, ni wajibu wa Waislamu kuonesha mfano bora wa maisha ya Mtume (s.a.w.w) kwa vitendo vya huruma, haki, uadilifu na kujenga jamii yenye amani na maridhiano.
Maulid hayo yamehitimishwa kwa dua maalum ya kuombea umoja wa Waislamu, amani ya taifa na ustawi wa jamii, sambamba na pongezi kwa waandaaji wote waliowezesha kufanyika kwa hafla hiyo kwa mafanikio makubwa.
Your Comment