Ibada ya pamoja (Jamaa) ya Dhuhri na Asr (n.k) katika Chuo cha Hazrat Zainab (sa) imekuwa mfano bora wa Chuo cha Maadili na utekelezaji wa mafundisho mazuri ya Kiislamu, ikiwa ni sehemu ya kujenga kizazi chenye maarifa, imani, na moyo wa ibada endelevu.

Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Katika Chuo cha Wasichana wa Kiislamu cha Hazrat Zainab (sa) - Kigamboni, Dar-es-salaam, Wanafunzi wamehudhuria ibada ya pamoja ya Swala ya Dhuhri na Al-Asr, ambapo Khatibu Sheikh Ghawthi amesisitiza katika hotuba yake umuhimu mkubwa wa kutekeleza ibada kwa wakati wake, hasa Sala tano za kila siku.
Amesema kuwa Sala ni nguzo kuu ya dini na darasa muhimu la malezi ya kiroho, inayomfundisha mwanadamu nidhamu, unyenyekevu, na utiifu kwa Mwenyezi Mungu (s.w.t). Kupitia Sala, mja huimarisha uhusiano wake na Mola wake na kupata utulivu wa moyo na mwanga wa ndani.

Allah (s.w.t) anasema katika Qur’ani Tukufu:
"Kwa yakini Sala humzuilia mtu kutokana na mambo machafu na maovu.” (Surat Al-‘Ankabūt, 29:45).
Khatibu aliongeza kuwa faida mojawapo ya kuswali mara tano kwa siku ni kumfanya mja kuwa daima katika hali ya ukumbusho wa Allah - kwamba kila tendo, kila kauli, na kila nia yake iwe ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu.

Aidha, Sheikh Ghawthi amesisitiza umuhimu wa kuswali kwa pamoja (jama’a) hasa miongoni mwa wanafunzi, akibainisha kwamba ibada ya pamoja hujenga umoja, upendo, na mshikamano wa kiroho, sambamba na kuimarisha maadili ya kijamii ndani ya taasisi ya elimu ya Kiislamu.
Mtume Muhammad (s.a.w.w) amesema:
"Salam ya pamoja ni bora kuliko sala ya mtu mmoja kwa mara ishirini na saba.”
(Imeelezwa katika Sahih al-Bukhari na Sahih Muslim).

Kwa hivyo, kuswali pamoja (katika Sura ya Jamaa) si tu tendo la ibada bali ni chuo cha maadili - kinachowafundisha wanafunzi utii, ushirikiano, na mapenzi ya Allah (s.w.t).

Kwa Mantiki Hiyo:
Ibada ya pamoja (Jamaa) ya Dhuhri na Asr (n.k) katika Chuo cha Hazrat Zainab (sa) imekuwa mfano bora wa utekelezaji wa mafundisho haya, ikiwa ni sehemu ya kujenga kizazi chenye maarifa, imani, na moyo wa ibada endelevu.
Your Comment