Katika mawaidha yake, Sheikh Abdul Ghani alisisitiza kuwa uongozi ni mhimili mkuu wa kusimama au kuporomoka kwa jamii yoyote. Alibainisha kuwa uongozi wa haki huijenga jamii, lakini uongozi wa dhulma huiangamiza.

Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt as -ABNA- Nakuru, Kenya: Waumini wa Kiislamu jijini Nakuru walijitokeza kwa wingi kushiriki Sala ya Ijumaa iliyoongozwa na Sheikh Abdul Ghani Khatibu, ambapo khutba ilijikita katika mada muhimu sana: Uongozi na nafasi yake katika mustakbali wa Ummah wa Kiislamu.
Katika mawaidha yake, Sheikh Abdul Ghani alisisitiza kuwa uongozi ni mhimili mkuu wa kusimama au kuporomoka kwa jamii yoyote. Alibainisha kuwa uongozi wa haki huijenga jamii, lakini uongozi wa dhulma huiangamiza.
Akinukuu Qur’an Tukufu, Sheikh alisoma Aya ifuatayo:
1. Aya ya Viongozi wa Haki
﴿وَجَعَلْنَا مِنْهُمْ أَئِمَّةً يَهْدُونَ بِأَمْرِنَا لَمَّا صَبَرُوا وَكَانُوا بِآيَاتِنَا يُوقِنُونَ﴾
(Surah As-Sajdah: 24)
“Na tukawafanya miongoni mwao viongozi wanaoongoza kwa amri yetu, kwa sababu walikuwa na subira na walikuwa wanaziamini Aya zetu kwa yakini.”
Sheikh alieleza kuwa Aya hii inaonyesha wazi kuwa uongozi wa haki unatokana na subira, imani thabiti na utiifu kwa Allah, si kwa nguvu, mali wala cheo. Viongozi halisi katika Uislamu huchaguliwa na Allah kupitia tabia zao njema, sio kupitia maslahi binafsi.

Sheikh Abdul Ghani alisisitiza kuwa uongozi ni amana kubwa kwa mujibu wa Qur’ani. Akinukuu Aya nyingine:
2. Aya ya Amanah na Uadilifu
﴿إِنَّ اللَّهَ يَأْمُرُكُمْ أَنْ تُؤَدُّوا الْأَمَانَاتِ إِلَىٰ أَهْلِهَا وَإِذَا حَكَمْتُمْ بَيْنَ النَّاسِ أَنْ تَحْكُمُوا بِالْعَدْلِ﴾
(Suratun-Nisaa: 58)
“Hakika Mwenyezi Mungu anawaamrisha mzirejeshe amana kwa wenyewe, na mhukumu kwa uadilifu mnapohukumu kati ya watu.”
Sheikh alibainisha kuwa kiongozi yeyote anayesaliti amana ya watu, huvunja amri ya moja kwa moja ya Allah. Uadilifu ni msingi wa kudumu kwa dola na jamii yoyote.
Katika sehemu nyingine ya khutba, Sheikh alizungumzia hatari ya uongozi wa dhulma kwa Ummah, akasoma Aya hii:
3. Aya ya Kuonya Dhulma ya Viongozi
﴿وَلَا تَرْكَنُوا إِلَى الَّذِينَ ظَلَمُوا فَتَمَسَّكُمُ النَّارُ﴾
(Surah Hud: 113)
Tafsiri ya maana: “Wala msiegemee kwa wale waliodhulumu, mkaguswe na Moto wa Jahannam.”
Sheikh alifafanua kuwa si tu viongozi wa dhulma wanaoadhibiwa, bali hata wale wanaowaunga mkono au kunyamazia uovu wao bila kuurekebisha.
Pia Sheikh alikumbusha wajibu wa waumini katika kuisimamia haki kupitia Aya hii:
4. Aya ya Kusimama Katika Haki
﴿يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا كُونُوا قَوَّامِينَ بِالْقِسْطِ شُهَدَاءَ لِلَّهِ وَلَوْ عَلَىٰ أَنْفُسِكُمْ﴾
(Suratun-Nisaa: 135)
“Enyi mlioamini! Kuweni wasimamizi imara wa uadilifu, mashahidi kwa ajili ya Allah, hata dhidi ya nafsi zenu wenyewe.”
Aya hii inaonyesha kuwa kulinda haki ni wajibu wa kila Muislamu, bila kujali cheo cha anayedhulumu.

Hadithi ya Mtume (saww) Kuhusu Uongozi:
Sheikh Abdul Ghani pia alinukuu Hadithi mashuhuri ya Mtume (saww):
«كُلُّكُمْ رَاعٍ وَكُلُّكُمْ مَسْئُولٌ عَنْ رَعِيَّتِهِ»
“Kila mmoja wenu ni mchungaji, na kila mmoja wenu ataulizwa kuhusu alichokichunga.”
Ufafanuzi:
Kiongozi ataulizwa kwa raia wake, mzazi ataulizwa kwa watoto wake, na kila Muislamu ataulizwa kwa nafasi yake katika jamii.

Mwisho wa Khutba
Sheikh Abdul Ghani alihitimisha kwa kuwausia waumini:
- 1_Waandae kizazi cha viongozi waadilifu.
- 2_Wasinyamaze mbele ya dhulma.
- 3_Waombe dua kwa ajili ya viongozi wema.
- 4_Waache tamaa ya dunia isiwaondoe kwenye misingi ya uongozi wa Kiislamu.
Mwisho aliomba: “Ewe Allah! Tupe viongozi wanaokuongopea, wanaohukumu kwa haki, na wanaotulinda na fitna za dunia.”

Your Comment