Maadhimisho ya kuzaliwa kwa Imam Mahdi (a.t.f.s) yaliyoambatana na 15 Shaaban yalifanyika tarehe 04/02/2026 mjini Moshi, Tanzania, kwa kushirikisha waumini wengi. Khatibu, Samahat Sheikh Miraji Salim, alieleza kwa kina neema ya uwepo wa Imam Mahdi (a.t.f.s) kama Baqiyyatullah katika ardhi ya Mwenyezi Mungu, na akawahimiza waumini kujiandaa kiroho na kimaadili katika kumngojea kwa vitendo, si kwa maneno pekee.
Shirika la Habari la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Mji wa Moshi, Tanzania, ulipambwa kwa nuru na furaha kubwa katika maadhimisho ya kuzaliwa kwa Imam Mahdi (a.t.f.s) yaliyofanyika tarehe 04/02/2026, sambamba na mnasaba mtukufu wa 15 Shaaban. Hafla hiyo ilihudhuriwa na waumini kutoka maeneo mbalimbali waliokusanyika kwa lengo la kuenzi na kukumbuka kuzaliwa kwa Khalifa wa Mwenyezi Mungu katika ardhi.
Mgeni rasmi na khatibu wa majlisi hiyo alikuwa Samahat Sheikh Miraji Salim, ambaye aliwasilisha darsa yenye kugusa nyoyo kuhusu nafasi na umuhimu wa Imam Mahdi (a.t.f.s) katika Uislamu. Sheikh Miraji alifafanua kwa kina kuhusu neema ya uwepo wa Imam katika zama hizi, akimtaja kama Baqiyyatullah, yaani hoja na akiba ya Mwenyezi Mungu kwa wanadamu.
Katika khutba yake, alisisitiza kuwa Imam Mahdi (a.t.f.s) ni alama ya matumaini, haki na uadilifu, na kwamba waumini wana wajibu wa kujiandaa kimaadili na kiroho ili kustahiki kuwa miongoni mwa wasaidizi wake wakati wa kudhihiri kwake. Aidha, aliwahimiza vijana kuuenzi Uislamu kwa vitendo, subira na mshikamano wa kijamii.
Hafla hiyo ilipambwa kwa qasida, dua, salamu Mahsusi kwa Imam Mahdi (a.t.f.s), pamoja na nasaha mbalimbali zilizolenga kuimarisha mapenzi ya Ahlul-Bayt (a.s) katika jamii. Waandaaji wa tukio hilo walieleza kuwa maadhimisho haya yana lengo la kuamsha fikra za Kiislamu, kuimarisha umoja na kueneza ujumbe wa amani na matumaini katika jamii.
Maadhimisho ya Moshi yameendelea kuwa mfano mzuri wa kuenzi misingi ya dini na kuhuisha kumbukumbu za viongozi wa haki, huku waumini wakiondoka wakiwa na ari mpya ya kumngojea Imam Mahdi (a.t.f.s) kwa vitendo na sio kwa maneno pekee.
Your Comment