Waumini wa Shia Ithna Ashari mkoani Arusha wameadhimisha Mazazi ya Imam Mahdi (a.t.f.s) katika Husseiniyyah ya Imam Ridha (a.s) chini ya uongozi wa Sheikh Maulid Hussein Sombi. Maadhimisho hayo yalipambwa na upandishaji wa bendera ya “Labbaika Ya Mahdi” kama ishara ya utii na mapenzi kwa Imam wa Zama.
Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Waumini na wafuasi wa Madhehebu ya Shia Ithna Ashari mkoani Arusha wameadhimisha kwa furaha na taadhima siku ya Mazazi Matukufu ya Imam Mahdi (a.t.f.s).

Maadhimisho hayo yamefanyika katika Husseiniyyah ya Imam Ridha (a.s) chini ya uongozi wa Samahat Sheikh Maulid Hussein Sombi, yakihudhuriwa na waumini kutoka maeneo mbalimbali ya mkoa huo.
Sherehe hizo ziliambatana na ibada, dua, qasida na mawaidha yaliyoeleza nafasi ya Imam Mahdi (a.t.f.s) katika uhai wa Umma wa Kiislamu kama Imam wa Zama na Khalifa wa mwisho katika mfululizo wa Makhalifa kumi na wawili wanaotokana na kizazi kitukufu cha Mtume Muhammad (s.a.w.w).
Tukio maalumu katika maadhimisho hayo lilikuwa ni upandishaji wa Bendera ya Imam Mahdi (a.s) yenye ujumbe wa “Labbaika Ya Mahdi”, ikiwa ni ishara ya utii kamili na ahadi ya kuendelea kumsaidia Imam wa Zama katika nyanja zote za kimaadili na kijamii.
Waumini walieleza kuwa tukio hilo linaakisi mapenzi, mshikamano na matumaini ya Umma wa Kiislamu katika kusubiri kwa vitendo ujio wa Sahibul-Asr Waz-Zaman (a.t.f.s), pamoja na kuimarisha maadili na mshikamano katika jamii.
Maadhimisho hayo yalihitimishwa kwa dua maalumu kwa ajili ya amani ya nchi, umoja wa Waislamu na kuharakishwa kudhihiri kwa Imam Mahdi (a.t.f.s).
Your Comment