Kikao cha 5 cha Kielimu kilichojadili mada ya “Mkombozi Katika Mitazamo ya Dini Mbalimbali: Tumaini la Viumbe Wote” kilifanyika tarehe 13 Februari 2026, kikiandaliwa na Jamiat Al-Mustafa International Foundation – Tanzania. Kongamano liliwakutanisha wanazuoni na wawakilishi wa dini mbalimbali kwa lengo la kuimarisha mshikamano, maridhiano na amani. Sheikh Dr. Alhad Mussa Salum, Mwenyekiti wa JMAT-TAIFA, alisisitiza kupinga ukabila, ubinafsi na umimi, na kuhimiza mazungumzo ya heshima kati ya dini. Alieleza kuwa dini zote zinapaswa kutambua udugu wa kibinadamu na kushirikiana kwa manufaa ya mustakabali mwema wa wanadamu. Pia aligusia dhana ya Mkombozi, akieleza nafasi ya Imam Mahdi (as) na Mtume Muhammad (saww) kama muombezi mkuu Siku ya Kiyama.

14 Februari 2026 - 22:39

Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Kikao cha 5 cha Kielimu kilichohusu mada ya “Mkombozi Katika Mitazamo ya Dini Mbalimbali: Tumaini la Viumbe Wote” kilifanyika Ijumaa, tarehe 13 Februari 2026, chini ya mpango na uratibu wa Jamiat Al-Mustafa International Foundation – Tanzania. 

Kongamano hili lilihudhuriwa na Wanazuoni, Wasomi, Wanafikra, na Watu Mashuhuri wenye fikra mbali mbali kutoka Dini mbalimbali, likiwa ni jukwaa la kujadili masuala ya kiimani na kijamii kwa mtazamo wa mshikamano na ushirikiano, Maridhiano na Amani.

Miongoni mwa waliohudhuria alikuwa Samahat Sheikh Dr. Alhad Mussa Salum, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT-TAIFA), aliye toa hotuba imara yenye msisitizo juu ya mshikamano na maelewano baina ya Dini mbali mbali, ikiwa ni Hotuba iliyohusiana na mada ya: “Mkombozi wa Ulimwengu na Mustakbali wa Ubinadamu.”

Sheikh Dr. Alhad Mussa Salum alianza hotuba yake kwa kupongeza fikra ya uwepo wa mkusanyiko kama huo uliokusanya watu wa dini mbalimbali, akisisitiza kuwa ni fursa muhimu ya kujadiliana na kushirikiana bila ubinafsi, umimi au ubaguzi wa aina yoyote. 

Alieleza kwamba Mwenyezi Mungu anatukataza kufurahia utengano, ukabila, ubinafsi, na umimi, na kwamba watu wanapaswa kuzungumza, kujadiliana, na kuafikiana kwa heshima.

Akiashiria mfano wa Iran, alibainisha kuwa kuna chombo maalum kilichoanzishwa na Kiongozi Mkuu wa Iran, Sayyid Ali Khamenei, kilicho na lengo la kuwaleta pamoja Waislamu wa Madhehebu mbalimbali na kuhakikisha wanashirikiana badala ya kuwa maadui, ili kulinda heshima ya Uislamu.

Sheikh Dr. Alhad Mussa Salum pia alisisitiza juu ya umuhimu wa kukutana na kujadiliana kati ya watu wa dini mbalimbali, akibainisha kuwa Waislamu na Wakristo wanatofautiana kidini, lakini wote ni ndugu wa kibinadamu.

Uislamu unasema tuwe na lugha nzuri katika mijadala; kutumia maneno makali kunaweza kupelekea kutengana. Alisema kwa msisitizo Sheikh Dr.Alhad Mussa Salum

Mkombozi - Atakayekuja Kuujaza Ulimwengu Haki na Uadilifu

Aidha, Sheikh Dr. Alhad Mussa Salum alikumbusha kuhusu Imam Mahdi (as) kama mtu anayehitajika kutambuliwa na Waislamu wa Madhehebu ya Ahlu-Sunna, ambaye atakuja kuujaza ulimwengu haki, usawa, na uadilifu, na kuondoa dhulma na batili. 

Alisisitiza kwamba Katika hatua ya juu ya zaidi ya Ukombozi, Mtume Muhammad (saww) ndiye Mkombozi Mkuu na wa Mwisho, ambaye atawaombea walimwengu wote Siku ya Kiyama na kuwa Muombezi Mkuu wa uokoaji wa Wanadamu kwa Siku hiyo nzito ambayo kila mja atahangaika ili kupata uombezi na ukombozi kutoka katika hali ngumu ya kusubiria hukumu ya Mwenyezi Mungu (SWT).

Mwisho wa hotuba yake, Sheikh Dr. Alhad Mussa Salum alibainisha kuwa mshikamano wa Kibinadamu na mijadala ya heshima ni msingi wa Amani, Maridhiano, na Mshikamano wa Binadamu, na kwamba Dini zote zina nafasi ya kutambua udugu wa Kibinadamu na kuleta matumaini na Mustakbali mwema kwa watu wote.

Your Comment

You are replying to: .
captcha